Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima (mwenye kofia nyeupe) akisalimiana na watumishi mbalimbali wa serikali mara baada ya kuwasili katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Gairo kwa ajili ya kikao cha utambulisho.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima Mei 24, 2023 ameanza kazi ya kuwatumikia wananchi wa Morogoro kwa kufanya ziara ya kujitambulisha Wilaya za Gairo, Kilosa na Mvomero.
Akiwa Wilayani Gairo, Mhe. Adam Malima pamoja na maagizo mengine ameiagiza Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Wilayani humo (GAUWASA) kwa kushirikiana na Bodi ya maji bonde la Wami – Ruvu pamoja na Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) kuhakikisha kuwa hadi kufikia Juni 30 mwaka huu mradi wa uchimbaji visima vinne vya maji baridi uliopo eneo la Kiswiti unakamilika na wananchi wanapata huduma hiyo ya maji.
Mhe. Adam Malima (katikati) akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo kwenye kikao cha utambulisho Wilayani humo, viongozi wengine ni Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa, Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Gairo pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
“...hakikisheni kwamba tunapofika tarehe 30 mwezi wa sita kutoka kwenye chanzo hicho na milioni mia mbili hizo, watu wa Gairo wapate maji japo hicho kiducho walicha ahidiwa, pesa za mama Samia zimekuja wapate hayo maji...” amesema Mhe. Adama Malima.
Amesema hakuna sababu yoyote ya kuwacheleweshea maji wananchi wa Gairo wakati Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshatoa fedha zaidi ya Tsh. Mil.200 kwa kwa ajiri ya Kukamilisha mradi huo.
Akiwa Wilayani Mvomero amewataka watendaji wote wa Wilaya hiyo Kila mmoja kwa nafasi yake kufuta sura mbaya iliyopo Wilayani humo ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji badala yake kujenga sura nzuri ya Wilaya kwa kuwa Wilaya hiyo ina mazuri mengi na fursa nyingi za uwekezaji kinachotakiwa ni kwa Kila Mtendaji kufanya kazi kwa weledi na kutoa Elimu kwa makundi hayo mawili.
Aidha, amewaagiza wakala wa huduma za misitu Tanzania TFS Wilayani humo kuja na mkakati mahsusi wa kupanda miti ya kutosha.
Akiwa Wilayani Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka Mkuu wa Wilaya hiyo amempongeza Mkuu wa Mkoa Mhe. Adam Kighoma Malima kwa kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kumwakilisha kutumikia nafasi ya Ukuu wa Mkoa Mkoani Morogoro.
Aidha, Mhe. Shaka amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya hiyo.
Ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa inaendelea kwa Wilaya zote Saba za Mkoa huo ambapo Mei 25 atafanya ziara Wilaya za Kilombero na Ulanga.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.