Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameonekana kusikitishwa na kitendo cha baadhi ya watendaji wa Serikali kuendelea kutoza ushuru wa mazao wakulima zaidi ya mara mbili jambo ambalo amesema ni kinyume na taratibu hivyo kuwaagiza Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri kuwataka watendaji wanaohusika na kusimamia makusanyo kuzigatia maagiz0 ya Serikali.
Martine Shigela ametoa maagizo hayo Mei 5 mwaka huu wakati akifungua kikao cha pili cha Baraza la Bisahara ngazi ya Mkoa kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Edema iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Amesema, bado kuna watendaji wanaotoza wakulima zaidi ya mara mbili ushuru wa mazao yao ya nafaka wanaposafirisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine na wengine kutoza ushuru kwenye mazao ambayo hayafikii tani moja jambo ambalo amesema ni kukiuka taratibu zilizopo.
“..kumeendelea kuwa na changamoto kwa baadhi ya halmashauri zetu, kuwa na tozo mara mbili hasa kwa mazao, mtu anatoa mpunga wake mlimba akifika Ifakara Mji anatozwa ushuru,anatoka Ifakara akifika Kilosa anatozwa ushuru…niwasihi watendaji wetu hasa wakurugenzi wa halmashauri kuwataka watendaji wetu wanaosimamia makusanyo wazingatie taratibu sheria ambazo zilishakwisha elezwa, serikali ya awamu ya sita imeendeleza kuweka misingi mizuri iliyowekwa na serikali ya awamu ya tano..” amesema Shigela
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa katika kikao hicho cha Baraza la Biashara amepongeza ushirikiano uliopo baina ya Ofisi yake na Sekta Binafsi hususan katika kuendelea kushirikiana na kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa muda mrefu baina ya pande hizo mbili.
Aidha, Martine Shigela ameshauri pande hizo mbili ziendelee kudumisha mahusiano hayo, kujipanga vema na kuhakikisha wanatumia kikamilifu jitihada zinazofanywa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za Kuifungua Tanzania hususan katika suala nzima la Uwekezaji.
Akiongelea eneo la uwekezaji la Star City lenye ukubwa wa ekari 6,000, Shigela amesema wameendelea kutatua changamoto za muda mrefu zilizokuwepo juu ya eneo la stsr city lililopo Nanenane Manispaa ya Morogoro ambalo lilikuwa limekwama na kwamba tayari eneo hilo limepimwa na kuanzia sasa viwanja vimeanza kuuzwa na kutumia fursa hiyo kuwakaribisha wanaohitaji maeneo kwa ajili ya uwekezaji.
Naye mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Morogoro Mwadhini Myanza pamoja na kupongeza ushirikiano uliopo baina ya Serikali na sekta binafsi amesema bado kuna changamoto ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi zikiwemo changamo za kodi nyingi kuingiliana na utekelezaji wa kanuni za Service levy.
Akichangia suala la service levy Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando amewashauri Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro kuwa makini katika kuchukua ushuru huo wa service levy ili wasichukue mara mbili kwa kutojua kutokana na mwingiliano wake badala yake wakae chini na kuainisha vema ili kuwafanya wahusika kulipa ushuru huo mara moja na hivyo kudumisha mahusiano baina ya pande hizo mbili lakini pia kwa kufanya hivyo wataongeza mapato hayo mara mbili.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.