Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ametishia kumfukuza kazi Mtendaji wa Mji Mdogo wa Mikumi Ndg. Mrisho Mrisho kutokana na kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya wananchi wanaogoma kutoa mchango kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ya Shule ya Sekondari Mikumi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani humo.
Loata Sanare amesema hayo Januari 10 mwaka huu ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule za Sekondari Mkoani humo ambapo kwa mara nyingine alirudi katika shule ya Sekondari ya Mikumi kukagua utekelezaji wa agizo alilolitoa Januari 6 mwaka huu la kukamilisha ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa kama limetekelezwa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sante akizungumza na Wenyeviti wa Vitongoji juu kukamilisha ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Sekondari Mikumi.
Kurudi kwa Loata Ole Sanare shuleni hapo kunatokana na taarifa kuwa baadhi ya wenyeviti wa Vitongoji wa Mji Mdogo wa Mikumi kutumia tofauti na malengo yaliyokusudiwa fedha za michango zinazokusanywa kwa ajili ya ujenzi wa Shule hiyo ikiwa ni pamoja na kuwalipia ada watoto wao kwa madai ya kurejesha fedha hizo baada ya watoto wao kupokelewa shuleni
.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare akitoa zawadi ya pesa kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kidoma Mlimani ambaye pia ni Makamu Menyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mikumi Bw. Salehe Tangula kwa kuhamasiha wananchi kushiriki katika maendeleo ya ujenzi wa shule ya Sekondari Mikumi.
‘’kuna pesa zimeliwa, kuna pesa zimekusanywa kwa wananchi na ndiyo sababu nagombana na watendaji, kwanini msikusanye, wengine wamekusanya wakasema tunawapeleka watoto wetu shule baadae tutakuja kupambana kutafuta pesa tulizokusanya” amesema Sanare.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amempongeza Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kidoma Mlimani ambaye pia ni Makamu Menyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mikumi Bw. Salehe Tangula kutokana na kazi nzuri ya kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na uhamasishaji wananchi kushiriki kazi za maendeleo, ukusanyaji wa michango kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuwasilisha kwa wakati fedha za michango kwa Kiongozi wake.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo akimpatia zawadi na mkono wa pongezi Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kidoma Mlimani ambaye pia ni Makamu Menyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mikumi Bw. Salehe Tangula kwa kazi nzuri ya uhamasishaji wananchi kushiriki kazi za maendeleo.
Loata amebainisha kuwa vyema kuwa mkali pale ambapo kiongozi anashindwa kutekeleza wajibu wake lakini pia kutoa pongezi na kusifia pale ambapo kuna jitihada za kutekeleza majukumu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Karibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo akiwasisitiza wananchi Mji Mdogo wa Mikumi kuwa wazalendo katika kufanya shughuli za maeñdeleo.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amewataka wananchi wa Mji Mdogo wa Mikumi kuwa na moyo wa uzalendo katika kujitolea kufanya shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa ambavyo hadi sasa unaonekana kusuasua.
Mhandisi Kalobelo amesema ni aibu kwa wananchi wa Mji wa mikumi kujenga msingi wa vyumba vya darasa kwa kutumia tofali za kuchoma badala ya kujengwa kwa mawe au matofali ya saruji huku akidai huko ni kukosa uzalendo na kutopenda maendeleo yao.
“…Watu hawapendi maendeleo yao tumeenda sehemu tumekuta misingi ya madarasa inajengwa kwa mawe au tofali za block, lakini hapa mmeokoteza haya matofali, na sehemu zote hata vijijini wamejenga madarasa mengi zaidi siyo Mjini kama hapa Mikumi…” amesema Kalobelo
Mwonekano wa ujenzi wa vyumba vya madarasa vya Shule ya Sekondari Mikumi ambao unapelekea Mkuu wa Mkoa Loata Sanare kuwa mkali kwa viongozi wa Mji Mdogo Mikumi kutokana na kutotimiza wajibu wao wa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.
Januari 6, mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare alimuagiza Mkuu wa polisi wa Wilaya ya Kilosa kuwaweka rumande wenyeviti wa vitongoji 21 katika Mji Mdogo wa Mikumi kwa kushindwa kuhamasisha wananchi kushiriki ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa vinavyohitajika kwa ajili ya wanafunzi 200 wa kidato cha kwanza wanaotarajiwa kuanza masomo yao Januari 11 mwaka huu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.