Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameagiza kufanyika upya zoezi la uhakiki wa nyumba za wananchi wa Kata ya Kihonda zilizoathiriwa na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ili kujua madhara yaliyojitokeza kwenye nyumba hizo na kisha waweze kulipwa fidia wanazostahili.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akizungumza na wananchi wa Kata ya Kihonda iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero mbzlimbzli za wananchi wa Kata hiyo Juni Mosi mwaka huu.
Martine Shigela ametoa agizo hilo Juni Mosi mwaka huu alipofanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kutatua kero za wananchi zinazowakabili hususan wa Kata ya Kihonda iliyopo katika Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (kulia) akiteta jambo na diwani wa Kata ya Kihonda Hamisi Kilongo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa huyo ya kutatua kero za wananchi iliyofanyika Juni Mosi Mwaka huu.
Martine Shigela amesema kuwa sio haki kuacha kuwalipa wananchi hao walioathirika na ujenzi huo wa Reli ya kisasa kwa kigezo tu cha kuangalia hadhi ya nyumba husika, na kwamba haziko kwenye kiwango kinachotakiwa kwani amesema kila mwananchi amejenga kulingana na uwezo alio nao.
“Mimi nakubaliana na wewe kwa yale yote ulioyaeleza, mamlaka ya Reli kuja kushirikiana na Mainjinia tulio nao kuhakiki upya nyumba kwa nyumba ili kujiridhisha kama kweli ilipasuliwa na SGR ni uamuzi sahihi na mimi nitalifuatilia kwa karibu ili tulimaliza mapema” amesema Shigela.
Kwa sababu hiyo, Martine Shigela ameiagiza Idara ya ardhi ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kushirikiana na wataalamu kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) watakaokuja ili kufanya tathmini ya nyumba ambazo zimeathirika pasipo kujali ubora wa nyumba zao bali kama nyumba hiyo imeathirika ili waweze kupata fidia zao.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi ambaye ni Kamanda wa Jeshi hilo Mkoa wa Morogoro Fortunatus Muslim akizungumza na wananchi wa Kata ya Kihonda wakati wa ziara Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela iliyofanyika Juni Mosi Mwaka huu.
Aidha Mkuu wa Mkoa amesema atawasiliana na Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo Mhandisi Masanja Kadogosa ili kuhakikisha wanaimaliza kero ya wananchi wa Kata hiyo huku akisisitiza kuwa kwa wale ambao nyumba zo hazijaathirika na ujenzi huo wa Reli ya SGR wasijiingize kwenye mchakato huo kwa kuwa sio haki na ni dhambi mbele mwenyezi Mungu kudanganya.
Sambamba na hilo Mkuu wa Mkoa ameitaka Idara hiyo ya Ardhi ya Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuanza mchakato wa kuwalipa fidia ya ardhi wahanga wote wanaostahili kulipwa fidia hiyo kutokana na changamoto ya double allocation changamoto ambayo amekiri kuwa imesababishwa na watendaji wa idara hiyo ya ardhi wasio waaminifu.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akiwa katika picha ya pamoja Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando (Kushoto mwa Mkuu wa Mkoa) pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Ally Machela (kushoto mwa Mkuu wa Wilaya wakisikiliza na kutatua kero za wananchi wakati wa ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa Juni Mosi mwaka huu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albart Msando ameeleza hatua zilizochukuliwa na Ofisi yake baada ya malalamiko ya wananchi juu ya kutolipwa fidia kutokana na mipasuko ya nyumba ikiwa ni pamoja na kutaka kujua sababu za kutolipa wananchi hao fidia na kuwaita wahusika, kukaa nao na suala ambalo bado anaendelea nalo kushughulikia ili kutouingiza mradi huo wa kimkakati kuwa mradi chechefu kwa wananchi.
Naye diwani wa Kata ya Kihonda Hamisi Kilongo amebainisha changamoto kubwa za Kata hiyo kuwa ni pamoja na ukosefu wa shule ya Sekondari, migogoro ya ardhi, tatizo la maji safi na salama pamoja na changamoto hiyo ya wananchi wa kata hiyo kutolipwa fidia baada ya nyumba zao kuathirika kutokana na ujenzi wa Reli ya mwendo kasi.
Nao wananchi wa eneo hilo akiwemo Magreth Helwa amemuomba Mkuu wa MKoa huo kujengewa soko kwani amesema kwa sasa wanapata mahitaji yao kutoka katika soko la Mawenzi au Soko Kuu la Mjini Morogoro ambapo ni umbali mrefu kutoka katika Kata yao.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Kihonda wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela alipokuwa akizungumza nao wakati ziara yake kusikiliza na kutatua kero za wananchi iliyofanyika Juni Mosi mwaka huu katika Kata hiyo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.