RC Morogoro akiri kuupokea Mkoa ukiwa tulivu
Mkuu wa MKoa wa Morogoro Fatma Abubakar Mwassa amekiri kupokea Mkoa huo ukiwa tulivu na kumpongea aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kurejesha Amani na utulivu ndani ya Mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa akipokea nyaraka kutoka kwa mtangulizi wale Martine Shigela ishara ya makabidhiano ya Ofisi hiyo
Fatma Mwassa ametoa kauli hiyo Agosti 16, 2022 wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya kiofisi baina yake na Mkuu wa Mkoa aliyepita Martine Shigela ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa amekiri kuwa amepokea Mkoa huo ukiwa shwari, tulivu na Salama.
“Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Geita nikushukuru tena na nikuthibitishie na niwathibitishie wadau wanaohudhuria makabidhiano haya kwamba nimeupokea mkoa ukiwa shwari kuna Amani na utulivu na wananchi wa Morogoro wanaendelea na shughuli zao kama kawaida za kujenga taifa” amesema Fatma Mwassa.
Wakuu wa Mikoa ya Morogoro na Geita wakiagana mara baada ya makabidhiano ya kiofisi yaliyoshuhudiwa na Mwenyekiti wa Chama Tawala (CCM) Mkoa wa Morogoro Drothy John (kulia)
Kwa sababu hiyo, amemshukuru mtangulizi wake Martine Shigela kwa kufanya kazi nzuri ya kuufanya Mkoa huo kuwa katika hali ya utulivu kwa kuwa amesema hakuna maendeleo yoyote yanayoweza kupatikana mahali popote bila kuwa na AMANI na UTULIVU.
makabidhiano
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka watumishi wa Umma kutenda haki wanapokuwa wameshika madaraka yoyote ambayo yanahusisha watumishi wengine chini yao, kusimamia misingi bora ya utumishi wa Umma na kuwa na utamaduni wa kuwalinda wafanyakazi wao.
Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo amekiri kuwa Mkoa wa Morogoro umepiga hatua kubwa kimaendeleo hususan katika Nyanja za kiuchumi na miundombinu ya barabara za lami, Masoko na miundo mbinu katika sekta ya Elimu na Afya ukilinganisha na miaka kumi ya nyuma.
Kwa Upande wake Martine Shigela pamoja na kutoa shukrani zake kwa viongozi na wananchi wote wa Mkoa wa Morogoro amemkumbusha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuendelea kulinda bonde la mto kilombero kwa kutekeleza maagizo ya Serikali yaliyotolewa kupitia timu ya Mawaziri nane waliokuwa wanashuhghulikia migogoro ya Ardhi hapa nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela
Wakuu wa Mikoa ya Morogoro na Geita wakiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro mara baada ya hafla ya makabidhiano
Shigela alibainisha maagizo hayo kuwa ni pamoja na kuweka mipaka ya bonde la Kilombero kwa kuzingatia mpaka wa mwaka 2017 kwa kuweka alama za kudumu, za kuonekana na za karibu zaidi ambazo zitawezesha wafugaji ama wakulima kutoingia na kufanya shughuli zozote za kibinadamu ndani ya bonde hilo tengefu.
Wajumbe wa Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro wakiwa katika picha ya pamoja na wakuu wa mikoa ya Morogoro na Geita mara baada ya hafla ya makabidhiano
Lakini pia amemwomba Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuendelea na zoezi la kugawa ardhi katika mashamba pori 11 yaliyofutwa umiliki wake na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika Wilaya za Kilosa na Mvomero hivyo ardhi hiyo kutakiwa kuwagawia wananchi wa maeneo hayo na sehemu ya ardhi hiyo kuwekwa akiba kwa ajili ya masuala ya uwekezaji.
Na mwisho, ni kumuomba kukamilisha zoezi la kuwafidia wananchi viwanja zaidi ya 3,000 ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro waliofanyiwa double allocation ili kupunguza kero za migogoro ya Ardhi kazi ambayo tayari Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa ameielekeza kuwa itasimamiwa na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya MKoa ili kuondoa udanganyifu unaoweza kujitokeza siku zijazo.
Akiongea kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya wenzake mara baada ya makabidhiano hayo kwa lengo la kutoa shukrani, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Majid Mwanga amesema Martine shigela amefanya mambo mengi ya kukumbukwa, huku akigusia lile la kufanikisha mbio za mwenge wa Uhuru za mwaka 2020 kuutoa Mkoa kutoka nafasi ya 29 hadi nafasi ya 9.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro Majid Mwanga akitoa shukrani wakati wa hafla ya makabidhiano baina ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa na mtangulizi wake Martine Shigela ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Geita
katika hafla hiyo fupi waandishi wa habari kutoka Mkoani humo nao walipata nafasi ya kupiga picha na wakuu wa mikoa hiyo miwili alama uwepo wa ushirikiano katika kazi zao
Aidha, amemkaribisha Mkuu wa MKoa wa Morogoro Fatma Mwassa, huku akisema kwamba yeye na Wakuu wa Wilaya wenzake wanaahidi kufanya kazi naye kwa kufuata maelekezo na maagizo atakayotoa kwa lipindi chote cha uongozi wake.
Kwa heri Martine Shigela, tunakutakie kazi njema, karibu Fatma Mwassa tuko tayari kukupa ushirikiano na kazi iendelee
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.