Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Morogoro ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Malima ameliagiza jeshi la Polisi Mkoani humo kuwakamata mara moja washukiwa wa na tukio la mtoto Yohana Lyanga (3) kuchomwa na maji ya mtoto sehemu ya makalio ambaye kwa sasa amelazwa katika kituo cha Afya cha Mtakatifu Joseph Wilayani Kilosa.
Mkuu wa Mkoa Adam Malima ametoa agizo hilo Agosti 30 mwaka huu wakati wa mahojiano na waandishi wa habari akiwa katika ziara ya kutembelea kiwanda kipya cha sukari cha Mkulazi na kukutana na Kadhia hiyo ambayo ameiita ni ukatili mkubwa na usiovumilika.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka amesema mtoto Yohana Lyanga amefikishwa Kituo cha Afya cha Mt. Joseph Wilayani humo Agosti 29 mwaka huu akiwa na majeraha maeneo ya makalio yaliyotokana na kuchomwa na maji ya moto.
Kwa sababu hiyo, Mkuu wa MKoa huyo amekemea vikali vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto vinavyotokea Mkoani humo na kwamba Serikali ngazi ya Mkoa haitasita kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaojihusisha au watakaojihusisha na vitendo hivyo.
“... ukatili kwa watoto hauna uhalali wa aina yoyote ile uwezi kuuhalalisha...ukatili kwa watoto, unyanyasaji wa wanawake, dhuruma dhidi ya watu masikini na vitu vyote vya ovyo ovyo vinavyo ondoa baraka katika Mkoa wetu lazima tuvipige vita...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema, hivi karibuni vitendo vya ukatili wa kijinsia hususan kwa Watoto kulawitiwa, kubakwa na kupigwa vimeongezeka katika Mkoa huo, hivyo amelaani vikali vitendo hivyo na kwamba Serikali itachukua sheria kali dhidi ya wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amesema Serikali inalaani vikali vitendo vyote vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kwamba vitendo hivyo ni kinyume na sheria za nchi ya Tanzania lakini pia ni vitendo vinavyoonesha kukosa ubinadamu.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka akimfariji mtoto Yohana Lyanga alipomtembelea hospitalini hapo kwa lengo la kujua hali yake.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali itagharamia matibabu ya mtoto huyo hadi pale hali yake itakapoimarika, pamoja na kugharamia matibabu hayo, Mkuu huyo wa Wilaya ameahidi kuwa Serikali itamlea mtoto huyo, itamsomesha na kumpatia huduma zitakazohitajika.
Naye, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Mtakatifu Joseph kilichopo Dumila Wilayani Kilosa Dkt. Selemani Sakoro amethibitisha kumpokea mtoto huyo Agosti 29 akiwa na majeraha sehemu za makalio na kubainisha kuwa hali yake kwa sasa inaendelea vizuri.
Tukio la Mtoto Yohana Lyanga limetokea katika Kata ya Msowelo Wilayani Kilosa ambapo alikuwa anaishi na ndugu zake akiwemo shangazi na Mjomba wake ambapo hadi sasa tayari shangazi na baba wa mtoto huyo wanashikiliwa na Jeshi la Polisi katika kituo cha Polisi cha Dumila kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Bi. Caroline Makemo mlezi wa Kituo cha watoto yatima kilichopo Dumila amejitolea kumuhudumia mtoto huyo hospitalini hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka akiwa pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo wakifanya mahojiano na watuhumiwa wa ukatili katika Kituo cha Polisi Dumila.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.