Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amempongezi mwanamasumbwi Twaha Kassim almaarufu kama Twaha Kiduku wa Mkoani hapa kwa ushindi alioupata wakati wa shindano lake la ngumi dhidi ya mpinzani wake kutoka nchini DRC lililofanyika hivi karibuni Mkoani Morogoro.
Mkuu wa Mkoa ametoa pongezi hizo Aprili 12 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo mara baada ya Twaha Kiduku kwenda kutoa shukrani zake kwa kiongozi huyo alizo kuwa anampatia kabla, wakati na baada ya pambano lake hilo.
Martine Shigela amesema, Mkoa wa Morogoro ni Mkoa wenye historia kubwa na ndefu katika Michezo mbalimbali ukiwemo mchezo wa ngumi na kwa mba Twaha Kiduku ameendelea kulinda heshima ya Mkoa huo na Taifa kwa ujumla katika kutetea Mataji mbalimbali ya Mchezo huo.
Kwa kutambua na kuthamini kazi anazozifanya Kiduku, Shigela amemuhakikishia Kiduku kuwa Serikali ya Mkoa huo itatoa kila aina ya sapoti ili kuhakikisha mazoezi na maandalizi kwa ajili ya mapambano mbalimbali yatakayopangwa siku za usoni.
“Nataka nikuhakikishie kwamba tutakupa kila aina ya Sapoti ili mipango yako unayotaka kuifanya na Mafunzo yako unayotaka kuyachukua pamoja na kambi utakayoiendesha basi kusiwe na changamoto yoyote. Kwa hiyo, nitakachohitaji mimi, uniletee mpango kazi wako ukoje, umekwama nini na unahitaji msaada gani ndani ya Mkoa ili kama Mkoa tuone namna gani ya kukusaidia”. amesema Mkuu Martine Shigela.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amemzawadia mwanamasumbwi huyo Tsh.1,000,000/= kama zawadi ya kufanya vizuri katika pambano lake lililofanyika Mkoani Morogoro.
Sambamba na Fedha hizo zilizotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Twaha Kiduku pia alizawadiwa Jumla ya Tsh. 1,100,000/= ikiwa ni zawadi kutoka kwa wadau wengine wakiwemo Wakuu ewa Wilaya za Mkoa huo waliomchangia wakati wa hafla hiyo ndogo ya kumpongeza kwa ushindi wake.
Kwa upande wake Bondia Twaha Kiduku ameushukuru Uongozi wa Mkoa wa Morogoro chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela kwa kuendelea kuwa pamoja nae katika mapambano yote anayoyafanya na kumpa sapoti ya hali na mali huku akiahidi kufanya vizuri kwa mapambano mengine ya ngumi yajayo.
Sambamba na ahadi hiyo Twaha Kiduku amebainisha siri ya mafanikio ya ushindi wake kuwa ni jitihada zake binafsi katika kufanya mazoezi, kufuata maelekezo ya mwalimu wake lakini zaidi Kumtanguliza Mungu kwa kila pambano ili amuwezeshe ushindi.
Kwa upande wake Mwalimu wa Bondia Twaha Kiduku ambaye pia amewahi kuwafundisha mabondia Francis Cheka na Cosmas Cheka Bw. Charles Mbwana, amesema kwa sasa wana miezi miatu ya kutetea ubingwa walio nao, kwa sababu hiyo wanaendelea kujifua kutete ubingwa huo kwa mpinzani yeyote atakayepatikana, huku akijinasibu kuendelea kuwapiga mabondia wa Jiji la Dar es Salaam.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.