Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Abubakar Mwassa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zaidi ya shilingi Bil.21 kwa lengo la kuboresha Sekta ya Afya Mkoani humo fedha ambazo zimeelekezwa kwenye ujenzi na ukarabati wa majengo ya kutolea huduma ya Afya.
Fatma Mwassa amemshukuru Rais Oktoba 19,2022 mara baada ya kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo ili kujionea mwenyewe ujenzi wa majengo mbalimbali yanayojengwa katika Hospitali hiyo pamoja na kuona huduma za Afya zinazotolewa kwa wananchi zinazotolewa na Hospitali hiyo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro Dkt. Daniel Nkungu akiwatambulisha madaktari wa hospitali hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa wakati wa ziara fupi hospitalini hapo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa mwaka huu wa fedha kupitia Halmashauri za Mkoa huo imetoa jumla ya Shilingi 18 Bil. kwa ajili ya kuboresha huduma za Afya huku Hospitali ya Mkoa ikipokea Shilingi Bil. 3 kwa ajili ya ujenzi wa majengo na ukarabati achilia mbali fedha zilizotolewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya Hospitali.
Muonekano wa jengo jipya la wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ya Rufaa Morogoro.
“Lakini nitumie fursa hii kwa niaba ya wananchi wote wa Morogoro kumshukurusa sana mama yetu mpendwa Rais wa awamu ya sita Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa upendeleo wa kipekee wanamorogoro kutuletea fedha nyingi za huduma za Afya kuboresha huduma za Afya katika Mkoa wetu” amesema Fatma Mwassa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa akimsikiliza Mganga Mfawidhi Dkt. Daniel Nkungu walipotembelea jengo la kuhudumia watoto njiti lililopo hospitalini hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa akiwa katika chumba cha CT-Scan kujionea namna mashine hiyo inavyofanya kazi.
Akiongea mbele ye vyombo vya habari mesema, hospitali hiyo imeboreshwa kwa kiasi kikubwa na huduma zinazotolewa kwa sasa ni za uhakika huku akitumia fursa hiyo kuwajulisha wananchi uwepo wa kipimo cha CT-Scan ambapo kwa mara ya kwanza imeletwa na Serikali ya awamu ya sita tangu kuanzishwa kwake mwaka 1946, hali inayowapunguzia wananchi gharama ya kusafiri nje ya Mkoa huo kutafuta kipimo hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akipanda mti mbele ya jengo la wagonjwa wa dharura wakati wa ziara yake hospitalini hapo.
Aidha, amesema hali ya upatikanaji wa dawa katika hospitali hiyo kwa sasa ni asilimia 98 hii ni kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma za Afya hapa nchini.
Katika hatua nyingine Kiongozi huyo amewataka wananchi wa wa Mkoa huo kupata matibabu ya awali katika Vituo vya Afya na zahanati vinavyopatikana katika maeneo yao kwa lengo la kupunguza foleni na gharama zisizo za lazima na kwamba lengo la uwepo wa Hospitali ya rufaa ni kuwahudumia wagonjwa waliopewa Rufaa kutoka maeneo mengine.
Mkuu wa Mkoa akisalimiana na wananchi waliokuwa wanasubiri huduma katika hospitali hiyo ya Rufaa Morogoro.
Lakini pia ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi wa Mkoa huo kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya iliyoboreshwa (iCHF) ili kupunguza gharama za matibabu pindi wanapougua kwa kujiunga pamoja na kupata Bima hiyo kwa gharama nafuu.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro Dkt. Daniel Nkungu amesema, pamoja na ujenzi wa majengo mengine hospitali hiyo inajenga jengo la kuchuja damu ambalo litawahudumia wagonjwa wenye matatizo ya damu na kuongeza kuwa kwa sasa huduma ya Watoto njiti inapatikana kutokana na uwepo wa jengo la kuwahudumia Watoto hao.
Muonekano wa jengo la huduma za dharura katika hospitali ya Rufaa Morogoro.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio amesema kuwa hospitali hiyo ya Rufaa inamahusiano mazuri na hospitali nyingine za binafsi ikiwemo hospitali ya Mtakatifu Francis iliyopo Ifakara Wilaya ya Kilombero Mkoani huo mahusiano ambayo yanahusisha pia kuwapeleka wataalamu kujifunza huduma ya mama na mtoto lengo ni kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo kwenye kikao na Mkuu wa Mkoa Fatma Mwassa.
Miongoni mwa miradi inayoendelea kutekelezwa Haospitali ya Rufaa ni pamoja na ujenzi wa jengo la huduma za dharura ambalo ujenzi wake umekamilika, jengo la wagonjwa mahututi linasubiri kukabidhiwa kutoka kwa mkandarasi, jengo la uchujaji wa damu ambalo lipo hatua za mwisho, jengo la Watoto njiti pamoja na miundombinu ya umeme.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.