Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za Afya kwa Wananchi wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla kwa kutoa fedha za kujenga vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akiwa na viongozi mbalimbali wakati akikagua ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Gairo.
Mhe. Adam Malima ametoa pongezi hizo Juni 12 mwaka huu wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Gairo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kwa Halmashauri zote Tisa za Mkoa huo lakini pia kushiriki mabaraza ya Madiwani kwa ajili ya kusimamia kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali - CAG.
Akiwa katika Hospitali hiyo Mkuu wa Mkoa amefurahishwa na huduma zinazotolewa hospitalini hapo hivyo akawataka Wahe. Madiwani wa Halmashauri hiyo na nyingine kuwa mabalozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuyasema hayo mazuri yanayofanywa na Serikari ya awamu ya sita.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima akimpa pole mtoto Devoth Julius (5) anayepata matibabu katika hospitali ya Wilaya ya Gairo baada ya kuumia Mguu wake akiendesha baiskeri.
"...Dkt. Samia amepeleka x- Ray kama hizi na hapa nimezikuta kama hizo zinafanya kazi, unajua sio kiini macho...sasa haya ndo mambo ambayo Mwenyekiti wa Madiwani mnawajibika kuyasema, kweli kabisa..." amesema Mkuu wa Mkoa.
Akiongelea suala la maji Wilayani humo Adam Malima amesema suala la maji ni changamoto kubwa kwa Gairo na inatakiwa kupatiwa ufumbuzi haraka.
Hapa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima anasikiliza kero ya uhaba wa maji kwa baadhi ya wanawake waliokuwa wanachota maji kwenye moja ya bomba Wilayani Gairo.
Kwa sababu hiyo ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na usafi wa Mazingira Wilaya ya Gairo (GAUWASA) kuhakikisha wanakamilisha upatikanaji wa maji kwa wakazi hao ndani ya miezi mitatu kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo ya kuchimba visima virefu na au kupata maji kwa njia ya mseleleko.
Moja ya mtambo wa kisasa wa kuchimbia visima virefu vya maji pamoja na mafundi wakiendelea na zoezi la uchimbaji wa visima vya maji katika eneo la Kisitwi Wilayani Gairo.
Hapa Mkuu wa Mkoa pamoja na viongozi mbalimbali wakiwa kwenye eneo ambalo uchimbaji wa visima vya maji unaendelea.
Sambamba na hayo Mhe. Adam Malima akiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani aliitaka Halmashauri hiyo kukusanya mapato kwenye sekta ya mifugo kwani amesema Sekta hiyo inakusanya 6% tu makusanyo ya ndani kupitia ushuru wa machinjio na ushuru wa mifugo wakati Sekta ya kilimo inakusanya mapato kwa 34% hivyo kuitaka Sekta hiyo iwe na mikakati ya ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri.
Picha mbalimbali za Wahe. Madiwani wakati wa Kikao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame amepongeza kasi ya Mkuu wa Mkoa katika utendaji kazi wake na kuahidi kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 wanakwemda kukusanya zaidi ya bilion moja ya mapato yasiyolindwa.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame (kulia) akimueleza jambo Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Mipango na Uratibu Bwa. Anza - Ameni Ndosa.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Rachel Nyangasi amebainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili Halmashauri yao kuwa ni pamoja na upungufu wa vyombo vya usafiri jambo linalochangia kushuka kwa mapato na kuwa na miradi kutokamilika kwa wakati sababu ya ufuatiliaji mdogo unaosababishwa na uhaba wa vyombo vya usafiri.
Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Gairo Mhe. Rahel Nyangasi akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakati wa Kikao Cha Baraza la Madiwani.
Nae Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi - CCM tawi la Kisitwi Bw. Godson Ngunei amemuomba Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa chama na Serikali kuunga mkono juhudi za Wananchi waliochangia ujenzi wa nyumba ya mganga wa zahanati ya Kisitwi ili iweze kukamilika kwa wakati, aidha, Mwenyekiti huyo amemshukuru Mkuu wa Mkoa na viongozi alioambatana nao kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo.
Mkuu wa Mkoa alikagua miundombinu ya barabara Wilayani Gairo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.