Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwasogezea karibu wananchi huduma za kibingwa kwa kupeleka madaktari bingwa katika ngazi ya Wilaya ili kuwapunguzia gharama wananchi wasio na uwezo wa kufuata huduma za Afya katika hospitali za Rufaa.
Mhe. Adam Malima amebainisha hayo Juni 3, 2024 alipokutana na madaktari Bingwa 35 maarufu kama Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kuripoti Mkoani humo tayari kuaza majukumu ya kuwahudumia wananchi wa Mkoa huo ukiwa ni mpango kabambe wa Mhe. Rais Samia wa kutaka Halmashauri zote 184 hapa nchini kufikiwa na madaktari hao Bingwa na kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi.
Mhe. Malima amesema, nje ya mpango huo, Serikali ya Mama Samia imefanya kazi kubwa katika sekta ya Afya kwani hadi sasa imepunguza vifo vinavyotokana uzazi kutoka vifo 556 kwa mwaka 2015/2016 hadi 104 mwaka 2021/2022 kwa kila Wanawake 100000 sawa na asilimia 81, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya viashiria vya afya ya uzazi (TDHS).
"... kuanzia miaka ya 2015 hadi 2020 tumetoka kwenye vifo 556 kwa kila akinamama 100,000 hadi 2022 kuwa na vifo 104 ni sawa na asilimia 81..." amesema Mhe. Adam Kighoma Malima
Sambamba na hilo, Mhe. Adam Malima pamoja na kuwapongeza madaktari Bingwa kwa kufanya kazi kubwa ya kuokoa uhai wa watu, amewataka kuendelea kutoa elimu ya lishe na chakula bora kwa wananchi, kwani amesema kuna uzalishaji mkubwa wa chakula kwa maeneo mengi ya Mkoa huo lakini bado elimu hiyo haijaenea kwa wananchi, hivyo amewataka kutoa elimu ya ulaji wa vyakula bora unaozingatia makundi yote ya vyakula.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Pindi Chana, aliyekuwepo katika tukio hilo muhimu la kuwapokea madaktari hao, alipopewa nafasi ya kusema neno kwa wananchi kutokana na jambo hilo kubwa analolifanya Dkt. Samia, amempongeza Rais Samia kwa kuongeza bajeti ya Sekta ya Afya huku akiwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara kama wanavyofanya check up ya vyombo vyao vya moto kila baada ya muda hivyo hivyo kwa mwanadamu badala ya kusubiri kuumwa ndipo uende hospitali.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wizara ya Afya Dkt. Ismail Mtitu amesema mpango huo ni wa wiki nane ambapo ulizinduliwa Mei 6, Mwaka huu Mkoani Iringa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) ambapo huduma hizo za kibingwa zitafikiwa hospitali zote 184 za Halmashauri zote za Mikoa 26 ya Tanzania Bara na kila Halmashauri itapokea madaktari bingwa 5 ili kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa wa idara ya nje na ndani katika hospitali husika.
Nae, Dkt. Joyce Gimonge ambaye ni Daktari Bingwa wa Watoto kutoka Mkoani Geita, kwa niaba ya madaktari wenzake amesema wananchi wanapaswa kuwahi matibabu mapema pale wanapohisi kuumwa ili kupata vipimo na kupewa matibabu ya haraka na hivyo kuokoa maisha yao.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.