Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amepiga marufuku kufanya maandamano yoyote ndani ya Mkoa huo yenye lengo la kupinga matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Loata Sanare amepiga marufuku hiyo Novemba 3 mwaka huu wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake akiwataka watanzania wote wakiwemo wa vyama vya siasa kukubaliana na matokeo yaliyotolewa ili wananchi waendelee na shughuli za kujiletea maendeleo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ndani ya Mkoa huo na Tanzania kwa ujumla ipo kwa ajili ya kulinda amani ya watanzania hivyo haitosita kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote au kikundi chochote kitakachojihusisha kwenye maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu.
“Tunasikia sehemu wanasema kuna maandamano endelevu ya kupinga matokeo ya uchaguzi, kwamba wasipoandamana tarehe mbili wataandamana siku nyingine….sasa nataka niwambie na mimi Mkoa wa Morogoro na nafikiri na Tanzania nzima ulinzi na usalama ni endelevu na yenyewe” Alisema Loata.
“Tuwaache watanzania sasa wafanye kazi za kujiletea maendeleo, tuwaache watanzania sasa waangalie matumaini makubwa yaliyotoka kwa Mhe. mgombea Urais laikini na ahadi za Wabunge na Madiwani, basi tuhangaike tuone watatufikisha wapi si suala la kuandamana tena” Alisisitiza Loata.
Sambamba na hayo, Sanare amewashukuru Wananchi wa Mkoa wa Morogoro kwa kutoa ushirikiano mzuri katika kipindi chote cha kampeini na uchaguzi kwa kuwa wasikivu, kufuata maelekezo ya Serikali na kudumisha amani wakati wote.
Pia, Loata Sanare amewataka wananchi wa Mkoa wa Morogoro kuwapa ushirikiano viongozi waliochaguliwa kwenye uchaguzi wa mwaka huu ili kuwasaidia kutimiza ahadi walizozitoa kipindi cha Kampeini huku akiwataka kujikita katika kujiletea maendeleo na kuachana na Maandamano kwa kuwa uchaguzi umekwisha.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.