RC morogoro ataka migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji ikomeshwe.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewaagiza wakuu wa Wilaya wote Mkoani humo kufanya tathmini ya Migogoro ya Ardhi katika maeneo yao na kuratibiwa na wakurugenzi ikiwa ni hatua za kukabilana na migogoro hiyo.
Mhe, Malima ametoa maaagizo hayo Septemba 27, mwaka huu alipofanya kikao na wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa huyo amesema kuwa yeye sio kwamba anapinga ufugaji bali anapenda kuona ufugaji wenye tija kwa Mkoa huo na sio ufugaji holela unaosababisha migogoro.
“watakwambia kwamba Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akataa Mifugo Morogoro Subhanallah naanzia wapi, mifugo inayofungwa na kuratibiwa vizuri ni uchumi mkubwa sana kwa Mkoa wa Morogoro lakini mifugo ambayo hairatibiwi ni disaster (janga) kwa Mkoa wa Morogoro” amesema Malima
Aidha, Mhe. Adam Malima amewataka viongozi hao Kwenda kuandaa mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ndogo zitakazotumika kulipa faini kwa mifugo itakayoharibu mazao ili kukomesha kabisa migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani humo kwani amesema kiwango cha faini kinachotumika sasa hakina uhalisia ukilinganisha na thamani ya fedha zinazolipwa kama fidia ya mazao yanayoharibiwa na mifugo hiyo.
Maagizo mengine aliyoyatoa Mkuu huyo ni Pamoja na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ukusanyaji wa mapato ya ndani, kusimamia mikopo ya asilimia kumi kukopeshwa kwa vikundi vinavyotambulika na kufanya ufuatiliaji na kurejesha fedha hizo kwa wakati.
Sambamba na maagizo hayo amewataka Wakuu wa Wilaya kuweka mikakati ya kukomesha migogoro ya kutengenezwa ndani ya wilaya zao kwa kuwa amesema hakuna migogoro inayoshuka kutoka angani isipokuwa migogoro hiyo inatengenezwa na kuwataka watu hao watafutwe na kuwajibishwa lakini pia amewataka wakuu hao kuweka mazingira wezeshi ya kujiandaa kwa kilimo cha mazao ya kimkakati.
Katika juhudi za kuimarisha na kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani humo Mshauri wa Jeshi la Akiba Mkoa wa Morogoro Kanali Valentine Makyao amebainisha mikakati aliyo nayo ya kutembelea kila Halimashauri za MKoa huo ili aweze kuboresha mafunzo ya jeshi hilo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe, Sebastian Waryuba kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo amemshukuru Mkuu wa Mkoa na kukiri kuyapokea maelekezo aliyoyatoa na kwamba yatatekelezwa kama ambavyo ameagiza.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.