RC Morogoro apiga ‘stop’ wananchi kuvamia Msitu wa Kuni, Atoa somo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa amepiga marufuku kwa mwananchi yeyote kuendelea kufanya shughuli za Kibinadamu ndani ya msitu wa Hifadhi unaojulikana kama msitu wa Kuni uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa upande Mwingine kwa kuwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria za uhifadhi.
RC Fatma Mwassa (Mbele) akiongea na baadhi ya wananchi wanaosadikika kuwa wamevamia Hifadhi ya msitu wa Kuni
Fatma Mwassa ametoa agizo hilo Septemba 15, 2022 baada ya kuanza ziara yake ya siku mbili katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kwa lengo la kujitambulisha, kutembelea miradi ya maendeleo pamoja na kutatua kero za wananchi ndani ya Wilaya ya Mvomero.
Amesema, msitu huo uko kisheria, hata hivyo kuna watu wanaendelea kuuvamia msitu huo na kujenga nyumba bila vibali halali, hali ambayo ni hatari kwao kwa kuwa wanafanya kosa na ni uhalifu kama uhalifu mwingine hivyo kuwataka wananchi hao wasiuze wala kununua eneo lolote ndani yam situ huo kwani wanatapeliwa.
“narudia tena kuwaambia, usinunue Ardhi wala kwa mtendaji wa Kijiji, wala kwa Mtendaji wa Mtaa wala kwa Mwenyekiti wa kijiji, hiyo Ardhi sio mali yao wao, mnapofanya hivyo mnatapeliwa” amesema Fatma Mwassa.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ametoa uelewa kwa wananchi waliofika eneo la msitu wa kuni kwa kuwaeleza utaratibu wa kupata kiwanja kwa kuzingatia sheria, taratibu na Kanuni na miongozo inayohusu Ardhi na si vinginevyo.
Akibainisha hilo Mkuu wa Mkoa Fatma Mwassa amesema ili kujenga nyumba ni lazima mwananchi awe ametekeleza mambo muhimu mawili: kuwa na hati miliki ya Ardhi na pili kuwa kupata kibali cha ujenzi wa nyumba anayotaka kujenga na vyote hivyo vinapatikana Ofisi za Ardhi za Halmashauri husika na sio kwa Mtendaji wa Kijiji wala Mtaa.
wananchi wa Eneo la msitu wa kuni wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro alipofika eneo la hifadhi kujionea namna lilivyovamiwa na wananchi
Aidha amemuagiza Afisa Mhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania {TFS} kuhakikisha wanalinda msitu huo na kuweka matangazo ya katazo la kujenga ndani yam situ huo na kuchora alama X au kuandika maneno ‘BOMOA’ kwenye majengo yote yaliyojengwa ndani ya msitu huo, huku akiwataka wananchi waliokwisha anza kuishi ndani ya Msitu wa kuni kutofanya chochote hadi pale watakapoambiwa vingine na Serikali.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.