Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare leo Januari 12 ametembelea Soko Kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ili kuona na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiasaha wa soko hilo.
Hatua ya Loata Sanare kutembelea soko hilo akiwa pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imekuja baada ya malalamiko kutoka kwa wafanybiashara wa soko hilo kuongezeka kila kukicha.
Moja ya Changamoto kubwa zilizojitokeza na kuelezwa na baadhi ya wafanyabiashara wakati wa ziara yake ni pamoja na vizimba vingi vya soko hilo kubaki bila wafanyabiashara ilhali kuna wafanyabiashara wengi wakihitaji vizimba hivyo.
Aidha, uwepo wa tozo kubwa kwa kila kizimba kwa mwezi imekuwa ni kero kwa wafanyabiashara hao ambapo kizimba kimoja kwa wafanyabiashara wadogo kimekuwa kikilipiwa shilingi 70,000 kwa mwezi badala ya shilingi 20,000 kwa mwezi bei ambayo imepangwa na Halmashauri hiyo.
Changamoto nyingine ni wateja kuwa wachache kufika sokoni hapo, soko kuwa mbali na kituo cha daladala hivyo wateja kupata changamoto kufika sokoni hapo na kukosekana kwa uzio katika soko hilo ni moja ya kero kunahatarisha usalama wa wafanyabiashara na mali zao.
Chanagamoto nyingine ni baadhi ya wafanyabiashara kuuza bidhaa zao nje ya soko hivyo kuzuia wateja kuingia ndani ya soko ili kuwafikia wafanyabiashara wenye vizimba wanaouza bidhaa kama hizo zinazouzwa nje ya soko.
Baada ya Mkuu huyo wa Mkoa kutembelea soko na kupokea kero za wafanyabiashara hao, alitoa maelekezo kwa wahusika ikiwa ni pamoja na kushughulikia kero zote zilizojitokeza.
Mkuu wa Mkoa Loata Ole Sanare ambaye pia ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Mkoa, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bakari Msullwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama ndani ya Wilaya kufuatailia kwa kina utaratibu wa ugawaji wa vizimba vya soko hilo kama ulifuata taratibu zote na unafuata makubaliano ya maamuzi ya vikao halali katika ugawaji wa vizimba hivyo.
’’Mkuu wa Wilaya unavyo vyombo vya kuthibitisha hilo, hao watumishi wa Manispaa ambao siyo waadilifu katika kusimamia kazi ya umma, wasiwe na nafasi katika kusimamia kazi hii, na siyo tu kusimamia, wasiwe na nafasi ndani ya Manispaa ya Morogoro’’ ameagiza Loata
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyabiashara wamemuomba Mkuu wa Mkoa Loata Ole Sanare kushusha kodi ya pango kwa wafanyabiashara kulingana na mzunguko mdogo wa wa biashara ilivyo kwa sasa.
Kwa upande wake Nataria Shirima amesema changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni uongozi wa soko hilo kuwakataza wafanyabiashara wa bidhaa za rejareja kufanya biashara mchanganyiko hali inayopelekea mazingira ya upatikanaji wa kodi kuwa mgumu.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Sheilla Lukuba ameeleza faida ya soko hilo itakayopatikana mara baada ya kuanza rasmi kutumika pamoja na kujibu kero ya tozo la kizimba kuwa kiwango hicho kimefuata uhalisia na gharma ya ujenzi wa soko.
Pia, Lukuba ametaja faida nyingine ya soko hilo ni Kuongezeka kwa mapato ya ndani kutoka 48 Mil kwa mwezi kabla halijavunjwa soko hadi 172.9 Mil kwa mwezi ambapo kwa mwaka soko hilo linatarajiwa kukusanya Shilingi Bil 2.07.
Soko Kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro limegharimu zaidi ya shilingi 17 Bil. hadi kukamilika kwake. Bil 10 zikitolewa na Serikali Kuu na Bil. 7.5 zikitolewa na benki ya dunia.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.