RC MOROGORO ATEUA KAMATI YA KUKAGUA ENEO SALAMA LA KUJENGA SEKONDARI KATA YA HOMBOZA WILAYANI MVOMERO.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameteua Kamati ya watu saba kwa ajili ya kukagua eneo la kujenga Sekondari ya Kata ya Homboza iliyopo Wilayani Mvomero baada ya eneo la awali lililokuwa limekubaliwa kujenga Sekondari hiyo kujiridhisha kuwa sio salama kwa wanafunzi watakaosoma shule hiyo.
Martine Shigela ameteua Kamati hiyo Machi 11 mwaka huu alipofanya ziara mahususi kwa ajili ya kuokoa fedha zaidi ya Shilingi milioni 470 zilizotolewa na Serikali na kutofanyiwa kazi kwa zaidi ya miezi miwili kwa sababu ya mivutano ya wapi shule hiyo ijengwe.
Kwa sababu hiyo Martine Shigela amefika kijiji cha manza Kata ya Homboza Wilayani Mvomero ambapo shule hiyo inatakiwa kujengwa ili kujiridhisha kama kuna mgogoro wa Ardhi unaochelewesha ujenzi wa shule hiyo na kujiridhisha mbele ya wananchi wa kijiji cha Manza kuwa hakuna mgogoro wowote wa Ardhi na kwamba kama kuna mwananchi ana mgogoro na eneo hilo aende mahakama.
“Yako maeneo masaa yote ni mgogoro tu, hata Ardhi isiyokuwa na mgogoro wanataka watengeneze mgogoro, na wengine wanataka Ardhi sio kwa ajili ya kujiendeleza, wanataka wachukue ili wakauze kwa watu wengine” amesema Martine Shigela.
“Kwa hiyo suala la Ardhi tumefunga, Kamishna wa Ardhi kama kutatokea mgogoro mwingine mwambie aende mahakamani” RC Shigela amesisitiza.
Katika Hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ameteua Kamati ya kwenda kukagua eneo ambalo limekubaliwa na wananchi kujenga shule ya sekondari baada ya eneo la awali kuonekana kutofaa ujenzi huo kwa kuwa ni chepe chepe na hatarishi kwa wananafunzi watakaosoma shuleni hapo.
Wajumbe hao ambao wamepewa siku mbili ya kufanya kazi hiyo na kutakiwa kuwasilisha taarifa yao kwa Mkuu wa Mkoa hapo Machi 14 mwaka huu ni pamoja na Afisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro, Afisa Mazingira wa Mkoa, Kamishna wa Ardhi wa Kanda ya Mashariki na Afisa Elimu wa Wilaya ya Mvomero.
Wajumbe wengine wa Kamati hiyo ni Afisa Tarafa ya Mlali na Afisa Ardhi wa Wilaya ya Mvomero wote wameagizwa kuambatana na Diwani wa Kata ya Homboza Hamidu Bakari Kalungwana kupitia eneo ambalo wananchi wameliteua kuwa mbadala wa eneo la awali ili kuona endapo eneo hilo linafaa kwa ujenzi huo ama la na kama halitafaa basi Kamati hiyo itafute eneo jingine lisilo na mgogoro wowote.
Wananchi wa Kijiji cha Manza wakiongozwa na Diwani wao Mhe. Mamidu Bakari Kalungwana amethibitisha kuwa eneo hilo halina mgogoro na uvumi kuwa eneo hilo lina mgogoro umetungwa tu na baadhi ya wananchi wasioitakiwa mema Serikali yao ambao muda wote wanatamani kuchochea vurugu.
Mhe. Kalungwana amesema wao walipendekeza eneo la awali kwa baada ya kuona lina nafasi kubwa zaidi ya Ekari 40 na kwamba shida kubwa ya eneo hilo ni mto ambapo kunatakiwa kujengewa kivuko na wao walikuwa tayari kujenga kivuko hicho hata hivyo wameshukuru maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kwamba wataungana na timu iliyoundwa ili kupata mwafaka wa suala hilo.
Kwa upande wake Sikitu Shomari Mkazi wa Kijiji cha Manza amekubaliana na maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ya kuunda kamati itakayopitia maeneo yote ili kupata eneo linalokidhi vigezo vya kujenga Sekondari yao huku Hamis Somba akimshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za kujenga sekondari ya watoto wao hivyo itapunhguza umbali wa Km zaidi ya 40 kufika shule waliyokuwa wanasoma awali.
Kwa upande wake Ndugu Simbamwene mwananchi wa kijiji cha Manza ambaye pia ndiye alijitolea eneo la ujenzi wa shule ya Sekondari amemuomba Mkuu wa Mkoa kupitia Kamati aliyoiunda kuendelea kufanya utafiti zaidi kuhusu eneo la awali kwa kuwa anaamini eneo hilo ni salama, changamoto yake ni kutokuwepo kwa karavati jambo ambalo anasema wananchi wanaweza kulijenga karavati hilo.
Machi 10 mwaka huu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI alifanya ziara ya siku moja ambapo pamoja na mambo mengine alifika katika Kijiji cha Manza na kukagua eneo la ujenzi wa shule hiyo ya sekondari na kutoa maelekezo kuwa eneo hilo sio salama kwa wanafunzi kwa kuwa ni eneo lenye maji maji na kutaka litafutwe eneo jingine.
Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepeleka shilingi milioni 470 katika Kata ya Homboza na baadae inatarajiwa kupeleka shilingi milioni 130 kwa ajili ya ujenzi Sekondari kuanza kujenga vyumba nane vya madarasa, jengo la utawala, Maabara na majengo mengine ujenzi ambao umecheleweshwa na mivutano ambayo tayari imekwishatatuliwa na Mkuu wa Mkoa.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.