Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amewataka waafanyabiashara wa Saruji Mkoani humo kuacha maramoja kupandisha bei ya saruji na badala yake kuuza bidhaa hiyo kwa bei ya awali kwa kuwa Serikali imejiridhisha hakuna sababu ya msingi ya kupandisha bei huku akiwaonya kuwa atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Loata Ole Sanare ametoa agizo hilo leo Novemba 23 mbele ya waandishi wa habari alipokutana na wafanyabiashara wa bidhaa hiyo Ofisini kwake na kuzungumzia hali ya bei ya bidhaa hiyo kabla na baada ya kupanda na kutoa maagizo yaSerikali.
Amesema, kabla ya bei ya saruji kupanda, Wilaya zilizopembeni mwa Mkoa wa Morogoro hususan za mbali kama Ulanga, bei ya Saruji mfuko mmoja ulikuwa unauzwa shilingi 15,000 hadi 16,000 na sasa ni shilingi 16,500 hadi 19,000, Wilaya ya Malinyi kabla bei kupanda mfuko mmoja uliuzwa shilingi 16,000 hadi 19,000 na sasa ni shilingi 16,500 hadi 20
.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa ameshangazwa na bei ya saruji kuuzwa kwa bei ya juu zaidi katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuliko hata Wilaya za mbali ambapo mfuko mmoja kabla ya kupanda uliuzwa shilingi 13,000 hadi 18,000 na sasa bei ya bidhaa hiyo inapatikana kwa shilingi 15,500 hadi 25,000 jambo ambalo amesema kufanya hivyo ni sawa na kuihujumu Serikali.
Kwasababuhiyo,Loata Ole Sanare amewaagiza wafanyabishara wote Mkoani humo kuunza saruji bei isiyozidi shilingi 16,000 kwa mfuko na atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria kwa sababu Serikali imejiridhisha hakuna sababu zozote za msingi za kupandisha bei ya saruji.
“Na kwa maana hiyo bei ya saruji itaendelea kuwa ileile bei ya awali….elfu kumi na tatu na mia tano kama ilivyokuwa awali na isizidi elfu kumi na sita, tumejiridhisha, hakuna sababu yoyote ambayo ni genuine (msingi) inayofanya bei ipande” .amesema Loata Sanare.
Aidha, amewashauri wafanyabiashara hao kuwa kama kuna sababu yoyote inayowafanya wapandishe bei ya saruji, nivema wakaijengea hoja sababu hiyo na kuiwasilisha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa naye ataiwasilisha hoja hiyo kwa viongozi wa juu ikiwemo Wizara husika.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza Maafisa waTRA Mkoa wa Morogoro kuwakagua wafanyabiashara wa saruji waliouza saruji zaidi ya shilingi 16,000/= kwa mfuko mmoja wapigiwe hesabu na kulipa fedha ya mapato ya ongezeko hilo la bei.
Nao wafanyabiashara wa saruji Mkoani humo walipohojiwa na vyombo vya habari juu ya ongezeko la beiwametoasababumbalimbalihukuBw. Thabiti Mohamed Islam akisema ongezeko hilo limetokana na uhaba wa bidhaa hiyo kiwandani kwa kuwa wateja wameongezeka hususan wakutoka nchi jirani ikiwemo Kenya na Jamhuri ya Kideokrasia ya Kongo ambako viwanda vyake vya Saruji vimefungwa kutokana na COVID – 19.
Hata hivyo Bw. Thabiti Mohamed ameishauri Serikali kutoruhusu wafanyabiashara wa nchi jirani kuchukua saruji hapa nchini ili bidhaa hiyo ipatikane kwa urahisi na hivyo kuzuia ongezeko la bei hiyo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.