Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ametoa siku 11 kwa Wenyeviti wa Mtaa na viongozi wengine wa Mji Mdogo wa Mikumi kusimamia zoezi la michango kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Mikumi na kukamilisha michango hiyo kabla au ifikapo Januari 31 mwaka huu.
Loata Sanare ametoa agizo hilo januari 19 mwaka huu katika ukumbi wa Mikutano wa VETA Mikumi wakati wa ziara yake ya siku moja katika Mji huo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vinne vinavyotakiwa kujengwa katika shule hiyo.
Aidha, Loata Sanare amewataka viongozi hao wahakikishe kila mwananchi anayestahili kutoa mchango anachanga kwa ajili ya ujenzi wa Shule hiyo kabla ya tarehe tajwa vinginevyo sheria kali dhidi yao zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kutiwa mbaloni.
Mkuu huyo wa Mkoa amewataka watendaji hao kutomuogopa mtu yoyote katika utendaji wao huku akisisitiza kutoa taarifa kwa mamlaka husika iwapo kunajitokeza hali ya uvunjaji wa sheria za kazi.
’’Acheni kuwa na nidhamu ya woga, wanakimbia kimbia kwa sababu Mkuu wa Wilaya anakuja, wanakimbia kimbia kwa sababu Mkuu wa Mkoa anakuja msifanye kazi kwa hali hiyo, fanyeni kazi kwa uadilifu fanya kazi kwa utaratibu unaotakiwa huna sababu ya kumuogopa mtu ’’ amesisitiza Sanare.
Akizungumzia suala la mapato katika Mji huo, Loata Sanare amebainisha kuwa wanahitajika watu waadilifu katika ukusanyaji wa mapato ili kusaidia kutekeleza shughuli za maendeleo katika Mji huo.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ametembelea Shule ya Msingi Mikumi Mpya iliyopo katika mji huo na kubaini upungufu wa madawati na vyumba vya madarasa kwa wanafunzi wa Shule hiyo.
Hali hiyo imebainishwa pia na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Ibrahim Chemba aliyekiri kuwepo kwa changamoto hiyo ambapo amesema inapelekea kupungua kwa ufanisi wa ufundishaji kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi kukaa chini na kubanana wakati wa kujifunza.
Kutokana na hali hiyo, Loata Sanare amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kumhamisha Shule Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Mikumi Mpya Ibrahim Chemba kutokana na kushindwa kuwa mbunifu katika kutatua changamoto za shule yake.
‘’Tafuta Shule nyingine, miaka mitano inakutosha hukutusaidia shule hii, ninakutoa kwenye Ualimu Mkuu kwa sababu umeshindwa kuwa mbunifu’’ amesema Loata.
Wakati huo huo wanafunzi wa Shule hiyo akiwemo Havintishi Juma ameiomba Serikali kutatua changamoto ya madawati na vyumba vya madarasa kutokana na kukaa wanafunzi zaidi ya 100 katika darasa moja.
Emmanuel Lazaro ambaye ni Mkazi wa Mikumi, ametaja changamoto inayopelekea wazazi kushindwa ujenzi wa miundombinu ya shule kuwa ni pamoja na dhana ya Elimu bure ambayo baadhi ya wazazi hushindwa kuielewa na kuitafisiri kuwa Serikali inafanya kila kitu bila kuwashirikisha wazazi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.