Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewaagiza wataalamu wa ardhi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kushughulikia kero za ardhi katika Kata ya Tungi iliyopo ndani ya Halmashauri hiyo na kupeleka mrejesho kwa Mkuu huyo wa Mkoa ndani ya siku tano.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akizungumza na wananchi wa Kata ya Tungi wakati wa ziara yake katika Kata hiyo Juni 9 Mwaka huu.
Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza hayo Juni 9 mwaka huu wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wananchi wa Kata ya Tungi katika Halmashauri hiyo.
Martine Shigela amesema hayo baada ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Tubuyu ‘B’ Bw. Ibrahim Maulid kuwasilisha kero ya migogoro ya idara hiyo ya ardhi iliyokithiri mtaani kwake, hivyo Mkuu wa Mkoa kutoa maagizo ya kushughulikiwa kwa haraka mgogoro huo ili wananchi waweze kujihusisha kikamilifu na shughuli za kimaendeleo.
“nimemuagiza Kamishna wa ardhi pamoja na wataalam wa Halmashauri kuifanyia kazi kero hiyo ndani ya siku tano na mniletee majibu juu ya malalamiko hayo” ameagiza Shigela.
Katika hatua nyingine Martine Shigela amemuagiza Meneja wa TARURA wilaya ya Morogoro kuhakikisha kero ya kufunguliwa kwa Barabara za mitaa katika Kata hiyo inashughulikiwa kikamilifu kwa kuzichonga Barabara hizo ili ziweze kupitika wakati wote na wananchi kupata huduma hiyo bila shida yoyote.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albaert Msando ameeleza baadhi ya changamoto za Kata ya Tungi zikiwemo uhaba wa upatikanaji wa maji safi na salama, uhaba wa madawati mashuleni pamoja na uchakavu wa majengo ya Shule za Msingi ambapo Serikali imeendelea kuchukua hatua ili kuzitatua changamoto hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albart Msando akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela kuzungumza na wananchi wa Kata ya Tungi wakati wa ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa iliyofanyika Juni 9 Mwaka huu.
Kwa upande wake diwani wa Kata hiyo Bw. Mchunguzi Namala pamoja na kuwasilisha changamoto za Kata hiyo pia ameishukuru Serikali kwa kuchukua hatua za kutatua changamoto ya maji kwa kutengeneza tenki kubwa lenye lita za ujazo 1mil, kulaza bomba za kusambaza maji hayo ambapo Kata ya Tungi inakwenda kuondokana na changamoto hiyo.
Nao wananchi wa Kata hiyo akiwemo mzee Musa Kasonga ameeleza ubovu wa Barabara za mitaa ya Kata hiyo ambayo imekuwa kero kubwa kwa wananchi, akieleza kuwa ipo baadhi ya mitaa barabara zake hazijafunguliwa na hivyo kutopitika kwa urahisi hali inayopelekea vifaa vya usafiri kama magari na pikipiki kuharibika mara kwa mara, kero ambayo Mkuu wa Mkoa alitoa maelekezo kwa wahusika ili kuishughulikia haraka.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.