Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wadau wa mazingira na misitu hapa nchini kupiga vita vyanzo vya uharibifu wa misitu ikiwemo uchomaji moto na ukataji holela wa miti na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Mhe. Malima amesema hayo Oktoba 3, 2024 wakati wa hafla fupi ya kufunga Jubilei ya miaka 50 ya mafunzo ya misitu hapa nchini iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mkoani Morogoro.
Mhe. Kighoma Malima amewataka wataalam wa utafiti wa misitu pamoja na maandiko mbalimbali wahayoandika amesema, bado kuna haja ya wao kwenda kutekeleza kwa vitendo yale waliyoyaandika kwani amesema uharibifu wa mazingira umeendelea kuwa mkubwa jambo ambalo linaongeza mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo ukame, mvua zisizo na uhakika, mafuriko na uharibifu wa mazingira.
" Nitoe wito kwa wadau wa misitu, kuhusu Suala la utunzaji wa Mazingira, tuondokane na tamadumi ya kuchoma misitu hovyo, tunachoma hadi sehemu zenye uoto wa asili, .." amesisitiza Mhe. Adam Malima.
Aidha, amekemea wale wote wanaoendelea kufanya shughulisha za kibinadamu pembezoni mwa mito na vyanzo vya maji kama kilimo, ufugaji na kufyeka misitu kuacha mara moja tabia hiyo kwani inaongeza uharibifu wa mazingira na akawataka watendaji wa Kata na Tarafa kutoa elimu kwa jamii juu ya utunzaji wa misitu.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuja na mkakati wa matumizi mbadala wa nishati safi ya kupikia utakaosaidia kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa kutokata miti hovyo kwa lengo la kuandaa mashamba na kupata mkaa na matumizi mengine ya kibinadamu.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima ameziagiza Halmshauri za Wilaya za Mkoa wa Morogoro kila moja kuwa na vitalu vya miche ya miti na kutenga ekari 200 kwa ajili ya kupanda miti ili wataalamu kutoka Chuo cha SUA kwenda katika maeneo hayo na kufanya utafiti wa aina ya miti inayostahili kupandwa.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Chuo Kikuu cha SUA Prof. Maulid Mwatawala, amesema katika kuongeza thamani ya misitu na kuongeza rasilimali watu, Chuo hicho kimejizatiti kuwa na kiwanda cha kuongeza thamani ya misitu kilichopo kampasi ya mazimbu Mkoani humo kiwanda ambacho kinahusika na uchakataji wa mazao ya misitu na kutoa mafunzo.
Naye Mkuu wa Ndaki ya Misitu, Wanyama pori na Utalii Prof. Agnes A. Shirima amebainisha kuwa misitu inaonekana ina mchango mdogo katika pato la Taifa jambo ambalo linatokana na biashara ya bidhaa za misitu kufanyika sehemu zisizo rasmi, hivyo ametoa wito kwa Serikali kutafuta namna ya kurasimisha biashara hiyo ili kuongeza pato katika sekta ya misitu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.