Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wakazi wa Mkoa huo hususan Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoani humo kutumia ujio wa wafanyabishara kutoka Comoro kuwa ni fursa ya kukuza biashara zao na kuitaka TCCIA kufungua milango ya Biashara na watu wa Comoro.
Mhe. Adam Malima ametoa kauli hiyo Julai 3 mwaka huu wakati akizungumza na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Comoro ambao wako Mkoani Morogoro kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi yao na Mkoa wa Morogoro.
Akifafanua zaidi, Mkuu huyo wa Mkoa amesema, nchi ya Comoro ina historia ndefu na ya siku nyingi ya kufanya biashara mbalimbali na Tanzania ikiwemo kufanya nayo biashara ya nyama, mchele, maharagwe na biashara nyingine hivyo amesema kuja kwa wafanyabiashara hao ni fursa ya kipekee kwa Mkoa huo.
“Tuione hiyo ziara ya wageni wetu kutoka Comoro kama ni fursa kubwa sana…” amesema Mhe. Adam Malima.
Akisisitiza zaidi kuhusu wafanya biashara hao kuwekeza Mkoani Morogoro, Mhe. Malima amesema, Mkoa huo una maeneo mengi na makubwa ya uwekezaji lakini pia una bahati ya kustawisha karibu kila zao ikiwemo zao la Karafuu, iriki, Vanila, kakaoa, pilipili mtama na bidhaa nyingine huku kisema Mkoa huo ni kinara wa kuzalisha mchele hapa nchini.
Katika hatua nyingine Kiongozi huyo amemtaka Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Morogoro Muadhini Mnyanza kufungua milango na wafanyabiashara hao huku akiwataka nao kujipanga Kwenda nchini Comoro kwa lengo la kuangalia fursa za kibiashara zinazopatikana huko.
Aidha, amesema kwa sasa watumie fursa ya ujio wao kufanya nao mazungumzo ya kina kuhusu sekta ya biashara na kuanza ushirikiano nao kwani amesema watu wa Comoro pia ni ndugu kihistoria na huku akiwashawishi kujifunza na kuongea lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wao Kiongozi wa Wafanya biashara hao kutoka Comoro Ahmed Rassoul amesema lengo la ziara yao Mkoani Morogoro kuona mazingira ya Mkoa huo na kubadilishana mawazo juu ya pande hizo mbili na kushirikiana katika sekta ya Biashara.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima (aliyevaa kanzu nyeupe, kibagharashia na miwani) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyabiashara kutoka Comoro kuja Morogoro kwa ziara maalum
Kwa upande wake Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga amesema atahakikisha wanafanya nao kikao na kuzungumza kwa kina kuhusu ushirikiano wa kibiashara na kuahidi kutoa ushirikiano kwao wakati wote watakapokuwa Mkoani hapa.
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Morogoro Muadhini Mnyanza amesema watafanya mazungumzo ya kina na ikibidi watawekeana makubaliano ya kibiashara kwa faida ya pande hizo mbili.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.