Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wanamorogoro kujitokeza kwa wingi kupima afya zao na kubaini mapema magonjwa yanayowakabili ili kupata matibabu bobezi yanayotolewa na Madaktari bingwa wa Rais Samia katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito huo Oktoba 15, Mwaka huu alipotembelea kambi ya Madaktari bingwa wa Rais Samia kutoka Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Aidha, Mhe Malima amesema kambi hiyo ilipanga kudumia wagonjwa 500 kwa siku nne lakini wananchi zaidi 300 wamejiandikisha kwa siku moja pekee ili kufanyiwa vipimo na kupewa ushauri wa kitaalamu na kuwasihi wananchi hao kwenda kuwaambia na wananchi wasio na taarifa ili waweze kupata fursa hiyo mapema.
"... hesabu ambayo wameshapatiwa matibabu ni zaidi ya 180 hivyo wananchi mnapaswa kujitokeza kupata matibabu kwa Madaktari hawa bingwa..." amesema Mhe. Malima
Sambamba na hayo, Mhe. Adam ameishukuru Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kutoa kibali kwa Madaktari hao kutoa huduma Mkoani humo kwani wagonjwa wanatoka sehemu mbalimbali za Mkoa huo zikiwemo Ifakara, Mvomero, Gairo na Morogoro DC hivyo kumefanya wananchi kuipenda huduma za Serikali yao.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili Dkt. Lemeri Mchome amesema wananchi wanapaswa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuepukana na magojwa yasiyo ya kuambukizwa ukiwemo ugonjwa wa shinikizo la damu, pia amewataka wananchi kuepuka shughuli kwa kiasi ili kuupa mwili muda wa kupumzika na kuendelea kuhifadhi kinga ya mwili.
Vile vile, Kaimu Mkurugenzi huyo amewataka wagonjwa mbalimbali hususan wanaosumbuliwa na mifupa, nyonga, miguu na mengine mengi kufika kambini humo ili kupata matibabu.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.