Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewasisitiza wananchi wa Wilaya ya Malinyi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura ili kuwa na haki ya msingi ya kushiriki katika uchaguzi wa mamlaka ya Serikali za mitaa.
Mhe. Malima amesisitiza hilo Oktoba 17, mwaka huu wakati wa ziara yake ya ufuatiliaji wa uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa Wilayani Malinyi kwa lengo la kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwa wingi.
Aidha, Mhe. Malima amebainisha kuwa wananchi wenye miaka 18 na kuendelea ndio wenye vigezo vya kujiandikisha bila kitambulisho chochote kwani kitambulisho cha mpiga kura hutumika katika uchaguzi mkuu ambao huhusisha chaguzi za Rais, Mbunge na Diwani hivyo amewatoa wasiwasi na kuwataka wanamalinyi kutumia siku zilizobaki kujiandikisha.
"... kama wewe ni mkazi wa njiwa huyo kiongozi utakayemchagua ndio atakayesimamia mambo yako kwa hiyo usiache kujiandikisha na kumtazama mtu anayekufaa..." amesisitiza Mhe. Adam Malima
Vile vile, Mhe. Adam amesema jukumu kubwa la wananchi ni kuchagua kiongozi wanaomtaka wao ifikapo Novemba 27 Mwaka huu ili kupata maendeleo bora katika vitongoji, mitaa na vijiji vyao hivyo kutokujiandikisha kutawanyima haki ya msingi ya kumchagua kiongozi wanaomkusudia.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi kutunza mazingira pamoja na uoto wa asili likiwemo bonde la mto Kilombero kwa kutokata miti hovyo kwa ajili ya shughuli za kilimo ambapo shughuli hizo hupelekea uharibifu wa vyanzo vya maji na kushindwa kuzalisha maji ya kutosha yanayoelekea katika bwawa la Mwalimu Nyerere linalotumika kuzalisha Umeme Kwa matumizi ya nchi nzima.
Kwa sababu hiyo amewataka wakulima kutumia njia mbadala ya kulima aina ya mazao ya miti ikiwemo miembe, michikichi, parachichi kwa lengo la kuzuia uharibifu wa mazingira ambapo amewataka wananchi wa kijiji cha Namhanga kata ya Iragua kutenga hekari mbili kwa ajili ya kuotesha miche 10,000 kwa kushirikiana na wataalamu wa kilimo wa Wilaya hiyo.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.