Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amemuagiza Mkuu wa Polisi Wa Wilaya ya Kilosa kuwaweka rumande wenyeviti 21 wa Vitongoji katika Mji mdogo wa Mikumi Wilayani humo kwa kushindwa kuhamasisha wananchi kushiriki ujenzi wa vyumba vinne vya madara yanayohitajika kwa ajili ya wanafunzi 200 waliofaulu mitihani ya darasa la saba mwaka 2020 na kutarajia kuanza masomo yao January 11 mwaka huu katika Shule ya Sekondari ya Mikumi.
Loata Sanare ametoa agizo hilo January 6 mwaka huu wakati wa ziara yake ya Siku tatu kukagua utekelezaji wa agizo la Serikali lililotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa la kutaka Wanafunzi wote waliofaulu mitihani ya darasa la saba 2020 kuwa madarasani mara Shule zitakapofunguliwa hivyo kila Mkoa umetakiwa kuhakikisha Wanafunzi hao hawakosi vyumba vya madarasa ya kusomea wala Madawati ya kukalia.
Hali ilikuwa sio ya kuridhisha sana Loata Sanare alipofika Shule ya Sekondari ya Mikumi ambapo wanafunzi 432 wamepangiwa katika Shule hiyo huku Wanafunzi 200 Kati yao kuonekana Kukosa vyumba vya madarasa manne huku kukiwa hakuna jitihada za makusudi zinazochukuliwa katika kukamilisha ujenzi huo hususan kwa wenyeviti wa Vitongoji wa Mji Mdogo wa Mikumi katika kuhamasisha wananchi, kushiriki ujenzi huo ambao bado uko hatua ya Msingi huku zikiwa zimebaki Siku tano tu kwa Shule zote kufunguliwa na Wanafunzi kuanza masomo yao na kuamua kutoa agizo hilo.
"...Hatukubaliani naye kabisa, OCD watendaji wote 21 ukimuondoa huyu niwakute wote kesho wapo ndani na wakija hapa watafanya Kazi ya kusomba wenyewe si wanashindwa kuwahamasisha watu wao, watakuja kushiriki wenyewe". ... amesema Sanare.
Aidha katika ziara hiyo Loata Ole Sanare amemuagiza Afisa Elimu wa Mkoa huo Eng. Joyce Baravuga kumuachisha nafasi ya Ukuu wa shule Mkuu wa shule ya Sekondari ya Kauzeni Mwl. Exavery Makaranga iliyoko katika Manispaa ya Morogoro kwa kutoonesha jitihada za dhati za kuendeleza ujenzi wa vyumba vya Maabara ambavyo vina zaidi ya miaka 13 bila kukamilika huku yeye akiwepo hapo kwa zaidi ya mika sita.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kauzeni Exavery Makaranga ambaye amesimamishwa nafasi ya Ukuu wa Shule hiyo.
Akiwa katika eneo la Shule hiyo Mkuu huyo wa Mkoa pia amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Sheilla Lukuba kumrudisha Mara moja Mtendaji wa Kata ya Kauzeni Jenipha Rashid ambaye yuko nyumbani kwa likizo na matazizo ya kifamilia kurudi Kazini Mara moja ili kuendelea na usimamizi wa Ujenzi wa vyumba vya madarasa wanavyodaiwa kwa ajili ya wanafunzi waliofaulu.
Mkuu wa Mkoa Loata Ole Sanare yuko katika ziara ya Siku tatu katika Wilaya za Morogoro, Kilosa, Kilombero na Malinyi kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa agizo la Serikali hususan ujenzi wa vyumba vya madarasa.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.