Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigella amewataka Wakuu wa Wilaya walioapa viapo vyao leo kuweka vipaumbele katika miradi ya kimkakati iliyoanzishwa Mkoani humo ili kuuletea Mkoa huo maendeleo ya haraka.
Shigella ametoa maagizo hayo kwa wakuu wa Wilaya hao Juni 21, mwaka huu katika viwanja vya Ikulu ndogo Mjini Morogoro wakati wa kuwaapisha Wakuu wa Wilaya watano walioteuliwa hivi karibuni na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Shigella amebainisha baadhi ya Miradi hiyo ya Kimkakati kuwa ni pamoja na Sehemu ya ujenzi wa kipande cha Reli ya mwendokasi – SGR kinachojengwa ndani ya Mkoa huo na mradi wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao hadi sasa upo katika hatua nzuri ya kukamilika.
Katika hatua nyingine, Shigela amewataka ma DC hao kuwafuata wananchi katika maeneo yao kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero wanazokumbana nazo ili kuuweka Mkoa huo katika hali ya usalama na kuleta maendeleo ya wananchi wake.
‘’Kero zipo nyingi sana na nyingine zimechukua muda mrefu sana bila kutatuliwa, kwanza tujenge misingi ya kuwasikiliza wananchi wanaolalamika na tusikilize watu wenye majibu ili tupime kati ya mlalamikiwa na mlalamikaji nani yupo sahihi’’ amesema Shigella.
June 18 mwaka huu, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya uteuzi wa Wakuu wa Wilaya nchini ambapo katika Mkoa wa Morogoro aliwateuwa Wakuu wa Wilaya watano ambao ni Jabil Makame (Gairo), Hanji Godigodi (Kilombero) na Halima Okashi (Mvomero).
Wengine walioteuliwa na Mhe. Rais na kuapishwa leo na Mkuu wa Mkoa huo wa Morogoro ni Albert Msando (Morogoro) na Majid Mwanga (kilosa) huku waliobakizwa kuendelea na majukumu ya Ukuu wa Wilaya zao za awali ni Mathayo Francis Maselle na Ngollo Ng’waniduhu Malenya wa Wilaya ya Ulanga.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.