Watu wawili wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa pamoja na Ofisi ya Kijiji kuchomwa moto Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro baada ya kuibuka vurugu zilizohusisha wananchi, viongozi wa Kijiji cha Ikwambi pamoja na askari wa jeshi la polisi Wilaya ya Kilombero huku chanzo kikidaiwa kuwa ni migogoro ya wakulima na wafugaji.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wananchi wa Kijiji cha Ikwambi, Kata ya Mofu wamesema wamelazimika kuchukua maamuzi ya kuwafungia ndani ya Ofisi baada ya malalamiko yao ya kunyanyswa na wafugaji na kulishia mifugo mashamba yao kutofanyiwa kazi na viongozi hao wa kijiji cha Ikwambi na Kata ya Mofu.
Akisoma changamoto za Kijiji hicho Bw. Gabrieli Haphrey Mapunda mkazi wa Kijiji cha Ikwambi amesema kijiji chao hakijasajiriwa kwa ajili ya wafugaji au mifugo bali kimesajiriwa kwa ajili ya wakulima pekee hata hivyo uwepo wa wafugaji kulisha mazao ya wakulima ndicho chanzo kilichopelekea wananchi wawili akiwemo ALLY MSOMA kupoteza maisha yao baada ya kuibuka vurugu baina ya makundi hayo.
Bwana Gabrieli Haphrey Mapunda mkazi wa Kijiji cha Ikwambi akisoma changamoto zinazowakabili mbele ya Mkuu wa Mkoa Fatma Mwassa.
Diwani wa Kata ya Mofu kilipo Kijiji cha Ikwambi GREYSON MGONERA amezungumza na mwandishi wa habari hii na kueleza kuwa siku ya tukio Oktaba 23 wananchi wenye hasira kali waliwakamata Viongozi wa Kijiji cha Ikwambi akiwemo Mwenyekiti wa kijiji Beatus Mitondo kwa tuhuma ya kushirikiana na wafugaji kuwaingiza katika Kijiji chao na hivyo kutaka kuwadhuru kwa kuwachoma moto.
Diwani anasema baada ya kuona viongozi hao wamefungwa Kamba na kufungiwa ndani ya Ofisi ya Kijiji hicho aliwasiliana na Askari Polisi ambao waliofika eneo la tukio haraka na kutaka kuwaokoa viongozi hao na kusababisha vurugu ambazo zimepelekea watu wawili kupoteza maisha.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Abubakari Mwassa akiongozana na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Morogoro wamefika katika Kijiji cha Ikwambi pamoja na kutoa pole kwa wafiwa ameahidi kuwaondoa ng’ombe wote walioko katika kijiji hicho cha Ikwambi, kwa kuwa amesema kuwa kijiji hicho hakijasajiriwa kwa ajili ya malisho ya Mifugo.
Aidha, amesema kutokana na tukio hilo anakwenda kuunda Kamati ndogo itakayohusisha vyombo mbalimbali vya Ulinzi na Usalama kwa ajili ya kuchunguza kwa kina tukio hilo na atapata nafasi ya kurudi Kijijini hapo kutoa taarifa rasmi kwao na kuchukua hatua stahiki kwa wahusika.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa kwa niaba ya Serikali amekabidhi ubani ikiwa ni pamoja na fedha taslim shilingi laki tano kwa kila familia iliyopatwa na msiba na vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi laki tano kwa kila familia na kufanya jumla ya shilingi milioni moja kwa kila familia iliyofiwa.
Hata hivyo Kiongozi huyo amewataka wananchi wa Kata ya MOFU kutojichukulia sheria mikononi, badala yake wanapoona kuna jambo ambalo haliendi sawa basi wafuate utaratibu uliopo wa kutoa taarifa kwa Viongozi wao wa Wilaya au Mkoa ama kumjulisha yeye kwa kumtumia ujumbe mfupi wa simu lakini sio kujichukulia sheria mkononi.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kilombero kuhakikisha migogoro yote inayojitokeza katika Wilaya hiyo kuitazama kwa jicho la pekee na kuishughulikia kikamilifu mara moja.
Aidha, kutokana na umuhim wa bonde la Kilombero kwenye mchango wa sekta ya nishati ya Umeme, Fatma Mwassa amefafanua kuwa asilimia 93 ya umeme unaotokana na maji hapa nchini unatoka katika vyanzo vya maji vilivyopo Mkoa wa Morogoro na kwamba watu zaidi ya Milioni 14 kutoka Mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro wanategemea Maji yanayotoka katika MKoa wa huo.
pia amesema dakio la maji linalokwenda kujaza maji katika Bawawa la J. K. Nyerere liko katika Bonde la mto Kilombero ikiwa ni pamoja na maeneo hayo ya Mofu, hivyo Serikali haiko tayari kuharibu vyanzo hivyo vya maji huku wakijua kuwa vyanzo hivyo ndivyo vinavyofanya bwawa la Mwl. Nyererekuwa endelevu, ndio tegemeo la chanzo cha Umeme na watu zaidi ya milioni 14 wanategemea maji ya kunywa kutoka bonde hilo.
Katika tukio hilo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imetoa ubani wa shilingi milioni moja kwa kila familia iliyopatwa na msiba, laki tano zikiwa ni fedha taslim Pamoja na vifaa mbalimbali kwa ajili ya msiba huo vyenye thamani pia ya shilingi laki tano.
Baadhi ya Vyakula vilivyokabidhiwa kwa wafiwa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa kwa niaba ya Serikali.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.