RC Morogoro awalalia macho Mameneja, Kituo cha Afya Kinonko.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amemuagiza Meneja wa Shirika la Umeme - TANESCO Mkoa wa Morogoro Mhandisi Fedgrace Shuma kufikisha huduma ya Umeme katika Kituo cha Afya cha Kinonko kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ili kurahisisha kituo hicho kuanza kutoa huduma ya Afya kwa wananchi wa eneo hilo kabla au ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
Martine Shigela ametoa agizo hilo Septemba 27 mwaka huu akiwa katika ziara ya siku moja ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kinonko kilichopo katika Tarafa ya mikese.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Gwata, Mkuu wa Mkoa Martine Shigela amesema Serikali imeleta fedha za kujenga majengo matano ya kituo hicho cha Afya sio kwa ajili ya kupendezesha watu au kwa ajili ya matumizi mengine bali yamejengwa ili kutoa huduma ya Afya kwa wananchi.
Aidha amefafanua kuwa wakati fedha hizo zinaletwa wakati wa erikali ya awamu ya tano Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo akiwa Makamu wa Rais alikuwa anamkumbusha mara kwa mara aliyekuwa Rais wakati huo na kipenzi cha watanazania hayati John Pombe Joseph Magufuli namna akina mama walivyokuwa wanapata tabu wakati wa kujifungua.
Kwa sababu hiyo, Mkuu wa Mkoa huyo amesema hakubaliani kukamilika kwa majengo hayo matano huku yakiwa hayatoi huduma ya Afya kwa sababu tu ya kukosekana kwa Umeme, Maji au Barabara na akatumia fursa hiyo kuagiza Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro na wataalamu wa Maji na Barabara kupeleka huduma hizo katika Kituo hicho cha Afya.
‘’… Na mimi nakubaliana na maelezo ya Mhe. Diwani umeme, maji na barabara yetu lazima iwe ndo kipaumbele chetu cha kwanza kuhakikisha kituo chetu kinafunguliwa haraka …’’ alisisitiza Martine Shigela.
“….haiwezekani Rais Samia atuletee fedha tukamilisha majengo haya, halafu sisi ambao tuliopewa dhamana ya kusaidia mambo madogo madogo haya yatushinde, haiwezekani”. Alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Kwa upande wa changamoto ya maji, Shigela amesema tayari Wakala wa Maji Mijini na Vijini - RUWASA pamoja na kuwa na mpango wa muda mrefu wa kusambaza maji katika kata hiyo ikiwemo Kituo hicho cha Afya, badoimetafuta imetenga Shilingi Milioni 30 kwa ajili ya kuchimba kisima cha maji ambacho kitasaidia kufikisha maji kituoni hapo na kutatua kero hiyo kwa muda hivyo amemuagiza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Morogoro Mhandisi Grace Lyimo kukamilisha mradi huo haraka ili kituo hicho kianze kutoa huduma kwa wananchi.
Akizungumzia suala la barabara, Shigela amesema hadi sasa Serikali ya Mhe. Samia Suluhu Hassan imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 1.5 kwa mwaka huu wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika Halmashauri ya Morogoro ukilinganisha na fedha Tsh. Mil. 200 zilizokuwa zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2020/2021 hivyo zitasaidia kujenga miundombinu ya barabara ikiwemo ya kuelekea kituo cha Afya cha Kinonko.
Diwani wa Kata ya Gwata Zongo lobe Zongo, amesema Kituo hicho cha Afya kinategemewa na wananchi kutoka Kata hiyo na kata nyingine za jirani hivyo kukamilika kwake kutasaidia kupunguza umbali mrefu wanaotembea wananchi wake na wa kata za jirani waliokuwa wanafuata huduma za Afya katika kata nyingine za Halmashauri hiyo.
Sambamba na hayo, Zongo amemuomba Mkuu wa Mkoa, kuwasaidia wananchi wa kata hiyo kutatua changamoto ya kutokuwa na mtandao wa simu ili kuondoa adha ya mawasiliano wanayokumbana nayo wananchi wake katika kuwasiliana na ndugu, jamaa na marafiki na kusaidia kuwarahisishia wananchi kwenye masuala ya kiuchumi.
Nao wananchi akiwemo Mariam Abdallah wa Kata ya Gwata amesema kutokuwepo kwa huduma ya umeme, maji na ubovu wa barabara katika kituo chao cha Afya cha Kinonko kumepelekea hadi sasa kituo hicho kushindwa kufanya kazi hivyo changamoto hizo kuzidi kuwarudisha nyuma kimaendeleo.
Mradi wa Kituo cha Afya Kinonko ulianza Septemba 2019 kwa gharama ya Shilingi Milioni 400 ikiwa ni ujenzi wa majengo matano ambayo ni jengo la nyumba ya mtumishi, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la Maabara, jengo la upasuaji na jengo la mama na mtoto.
Mradi wa Kituo cha Afya cha Kinonko Katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ulianza Septemba 2019 kwa gharama ya Shilingi Milioni 400 ikiwa ni ujenzi wa majengo matano ambayo ni jengo la nyumba ya mtumishi, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la Maabara, jengo la upasuaji na jengo la mama na mtoto.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.