Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amesema Wilaya ya Ulanga ina madini mengi yenye thamani kubwa yakiwemo madini ya Rubi Pamoja na vivutio vingi vya utalii, na kuwataka watu kutoka ndani na nje ya nchi Kwenda wilayani Ulanga kuwekeza katika sekta hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa akihutubia wananchi Wilayani Ulanga kwenye Uzinduzi wa tamasha la Uwekezaji linalojulikana kama Iherepa 2.
Mhe. Fatma Mwassa ametoa rai hiyo Novemba 19 mwaka huu kwenye uzinduzi wa Tamasha la Uwekezaji linalojulikana kama Iherepa 2 lililofanyika Wilaya ya Ulanga, Mkoani humo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amesema utajiri uliopo kwenye Wilaya hiyo unaotokana na wingi wa aina mbalimbali za madini yenye thamani kubwa hivyo kuvutia wageni wengi kutoka nje ya Wilaya hiyo na mzunguko mkubwa wa fedha zinazotokana na uchimbaji wa madini au utalii katika Wilaya hiyo.
Hapa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa anasikiliza ufafanuzi wa uchimbaji madini kutoka kwa wataalamu wa madini kwenye banda mojawapo yaliyoshiriki kwenye tamasha hilo la Iherepa.
“...lakini kuzinduliwa kwa jambo hili kunatoa fursa kwa wageni wengi kuja, kwanza kufanya utalii, kwa sababu idea hii ya ku connect madini na utalii imekuwa ni kitu kipya kwa eneo hili na kwa watanzania wengi...” amesema Fatma Mwassa.
Mkuu huyo wa Mkoa ameongeza kuwa Wilaya hiyo imebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii vya kipekee na kuifanya Wilaya hiyo kuwa ya kipekee kupitia Sekta hiyo ya utalii, vivutio hivyo ni Pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ambayo imesheheni baianuai ya kuvutia.
Muonekano wa nje wa jengo la kitalii ambalo limejengwa na kunakishiwa kwa miamba ya mawe .
Muonekano wa ndani wa jengo la kitalii ambamo kuna samani za kuvutia zilizotengenezwa kutokana na mawe yaliyochongwa yanayotokana na miamba iliyopo eneo hilo.
Aidha, Mhe. Fatma Mwassa ametumia tamasha hilo kusisitiza Halmashauri zote Mkoani humo kutunza mazingira kwa kupanda miti Zaidi ya milioni moja kwa kila mwaka ili kurudisha uoto wa asili na majira ya mvua kunyesha inavyotakiwa.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mhe. Salim Hasham, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Ruby International, kwa kujitoa na kuwekeza katika sekta ya Madini Wilayani humo.
Mhe. Fatma Mwassa akimpongeza Mhe. Salim Hasham Mbunge wa Jimbo la Ulanga ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ruby International kwa kuwa mzalendo kuwekeza katika Jimbo lake.
Mhe. Majid Mwanga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa akiwa pamoja na Mhe. Mathayo Maselle Mkuu wa Wilaya ya Malinyi.
Katika hatua nyingine amempongeza Mbunge huyo kuwa na nia ya kuwa mchimbaji mkubwa wa madini na kuwainua wachimbaji wadogo anaofanya nao kazi hiyo kwa kuwawezesha kuchimba kisasa.
Kwa upande wake Mbunge wa Ulanga Mhe. Salim Hasham amesema wamejipanga kuhamasisha utangazaji wa fursa za uwekezaji zilizopo katika Wilaya hiyo na Mkoa kwa ujumla, pia amesema wanatarajia kukuza sekta ya kilimo kwa kulima mazao ya kimkakati.
Nae Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro Paul Ngwembe ameomba kuwepo ushirikiano na mhimili wa mahakama kwakuwa wote wanalenga kujenga jamii isiyo migogoro, ameongeza kuwa wako mbioni kujenga Mahakama za Wilaya za kisasa za ulanga, Malinyi na Kilosa, na baada ya miaka miwili Wilaya zote ndani ya Mkoa huo zitakuwa na Mahakama.
Mhe. Fatma Mwassa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akiwa pamoja na Mhe. Paul Ngwembe Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro.
Tamasha hilo la Ulanga Iherepa limeambatana na shughuli mbalimbali ikiwa ni Pamoja na maonesho ya utalii, uchimbaji madini, michezo ya mbio za baiskeli milimani na utalii wa mbuga ya Mwalimu Nyerere.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa akitoa vyeti vya pongezi kwa washindi na washiriki mbalimbali katika tamasha hilo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.