Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Abubakar Mwassa ametembelea kiwanda cha kusindika mazao aina ya kunde na kuahidi kutoa ushirikiano na kutatua changamoto zinazokikabili kiwanda hicho.
Mhe. Mwassa amesema hayo Aprili 11, 2023 alipotembelea kiwanda cha Mahashree Agro Processing Ltd kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ikiwa ni utekelezaji wa lengo la Serikali la kuondoa kero zinazowakabili wawekezaji na kuvilinda viwanda kwa faida ya pande mbili yaani wananchi na wawekezaji.
Akijibu changamoto Mhe. Fatma Mwassa ameahidi kuwakutanisha wataalamu, wakulima na viongozi wa kiwanda hicho ili kuweka mikataba yenye faida kwa pande zote mbili na kutoa uelewa kwa wakulima kuuza mazao yao katika kiwanda hicho kwani nje ya kusaidiwa mbegu za mazao hayo, bado kiwanda hicho ni mkombozi kwao kwa maana ya soko la kuuza mazao yao.
Akizungumza mara baada ya kumpokea Mkuu huyo wa Mkoa, Meneja wa Kiwanda hicho Bw. Kamalesh Maheshwari ametaja changamoto inayokabili kiwanda hicho kuwa ni pamoja na wakulima wa mazao ya mikunde kutouza mazao yao katika kiwanda hicho, pamoja na kusaidiwa mbegu na kiwanda, wakulima hao wakati wa mavuno hurubuniwa na walanguzi na kuuza mazao yao kwao.
Kiwanda cha Mahashree Agro Processing Ltd kinachouza mazao yaliyosindikwa nje ya nchi zaidi ya 40 duniani, kinajihusisha katika kununua, kusindika na kupaki mazao aina ya mikunde yakiwemo mbaazi, Ufuta, kunde, choroko na dengu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.