Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Abubakar Mwassa amewataka Wakala wa misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kilombero kusitisha mara moja utoaji wa vibali vya kukata miti ili kunusuru dakio la maji la mto kilombero huku akimtaka Mkuu wa Wilaya hiyo Hanji Godigodi kusimamia katazo hilo kwa kuwa ndiye mwenyekiti wa utoaji wa vibali hivyo.
Fatma Mwassa ametoa katazo hilo Januari 18 mwaka huu wakati akizindua kampeni ya upandaji miti kwenye vyanzo vya maji iliyofanyika kando ya Mto Lumemo mjni Ifakara Wilayani Kilombero Mkoani humo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutunvyanzo vya maji na kuvilinda alilolitoa wakati wa hafla ya ujazaji maji Bwawa la J. K. Nyerere.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema TFS mwaka huu walipanga kupanda miti milioni moja na laki tano lengo ambalo bado halijafikiwa huku kasi ya ukataji miti ikiwa ni kubwa kuliko ile ya upandaji miti, kwa sababu hiyo amesema haoni sababu ya kuendelea kutoa vibali vya kukata miti na kutaka vibali hivyo kusitishwa ili kunusuru dakio la maji la Kilombero ambalo mto huo unaochangia asilimia 65 kujaza maji katika bwawa la Mwalimu Nyerere.
“nisisitize tena TFS, hakuna mambo ya kutoa vibali Kilombero vya kukata miti, umeshindwa kupata miche milioni moja na laki tano ya kupanda, kwa sababu hiyo hatuwezi kukata, kwa sababu kasi ya kukata miti ni kubwa kuliko ya kupanda miti hivyo kuathiri dakio hilo ambalo limekwisha athiriwa kwa asilimia 80” ameagiza Fatma Mwassa.
Aidha, amewataka watu wa Bonde kwa mamlaka waliyonayo kutoa vibali vya matumizi ya maji na kuhakiki mara kwa mara ili kujiridhisha kuwa vibali vilivyotolewa vinatekelezwa kwa mujibu wa masharti yaliyotolewa, lakini vibali hivyo pia vizingatie upatikanaji wa maji na uendelevu wake badala ya kutoa vibali vilivyopitiliza na hivyo kuathiri upatikanaji wa maji hususan katika Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa huo wakishirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri zao kuwasaka wazazi wote wa watoto waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza na hawajaripoti shuleni kuwakamata na kuwachukulia hatua stahiki ili watoto hao wapelekwe shuleni kwa kuwa hiyo ndiyo haki yao ya kwanza na ya msingi. Akifafanua zaidi Fatma mwassa kwa mshangao mkubwa amesema pamoja na serikali kufikia hatua ya kutoa Elimu hiyo bila malipo bado watoto wengi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza hawajaripoti shule zaidi ya asilimia 50 kwa kisingizio cha kukosa sare za shule na madaftari jambo ambalo amesema halikubaliki.
Akieleza umuhimu wa Bonde la Rufiji, Afisa wa Maji Bodi ya Maji Bonde la Rufiji dakio la Kilombero Mhandisi Emannuel Lawi amesema Bonde la Mto Kilombero linachangia asilimia 15 – 18 ya pato la taifa (GDP) kupitia sekta za Kilimo Ufugaji Nishati na Utalii.
Hata hivyo ametaja changamoto kubwa zinazowarudisha nyuma wakati wa uendelezaji wa Bonde hilo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa shughuli za Kilimo katika vyanzo vya maji na kingo za mito na kuhatarisha mito hiyo na baadae kuhatarisha mipango ya taifa ukiwemo mradi mkubwa wa Bwawa la Julius Nyerere.
Changamoto nyingine nyingine aliyoitaja Mhandisi Lawi ni uwepo wa makundi makubwa ya mifugo katika mito na vyanzo vya maji ambayo husababisha vyanzo hivyo kukauka kabisa.Changamoto nyingine ni kutupa taka kwenye mito na baadhi ya wavuvi kudiliki kukata miti iliyopo kando ya mito.
Kwa upande wa TFS Wilaya ya Kilombero wamesema tayari wana miche ya miti zaidi ya elfu hamsini ambayo watagawa bure kwa wananchi kwa ajili ya kupanda katika maeneo mbalimbali lengo ni kutunza mazingira na miche mingine itapandwa katika maeneo ya misitu yao iliyoharibiwa na kuahidi kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa Mkuu wa Mkoa katika hafla hiyo.
Nao wananchi walioshiriki zoezi hilo la upandaji miti akiwemo Fadhiri Mwanawaga Mjini Ifakara amesema miti ni muhim kwa binadamu kwani inasaidia uwepo wa Mvua lakini pia miti ya biashara kama vile mitiki na kokoa inasaidia kuwapatia kipato kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.