RC MOROGORO ATAJA MAFANIKIO YA SERIKALI SEKTA YA ELIMU, ATAKA WATOTO WA JAMII YA WAFUGAJI KUANDIKISHWA SHULE.
Serikali ya awamu ya sita katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetumia zaidi ya shilingi Bil.38 kwenye Sekta ya Elimu Mkoani Morogoro kuboresha miundombinu mbalimbali ya kujifunza na kujifunzia kwa lengo la kuboresha Sekta ya Elimu Mkoani humo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Aboubakar Mwassa Septemba 9 mwaka huu wakati wa uzinduzi wa vitabu vya miongozo ngazi ya Mkoa vilivyotolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI vikiwa na lengo la kuboresha Elimu kwa ngazi ya Msingi na Sekondari.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Abourbakar Mwassa akiongea na wadau wa Elimu siku ya uzinduzi wa Vitabu, Septemba, 9, 2022
Akiongea na wadau wa Elimu wa Mkoa huo wakiwemo walimu, Ukumbi wa TANZANITE katika Halmashauri ya Manispaa ya Morooro, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haina budi kupongezwa kwa kazi kubwa ya kuboresha Elimu katika Mkoa huo.
RC Fatma Mwassa (kulia) akizundua vitabu vya miongozo, kulia kwake ni Dkt. Mussa Ali Mussa Katibu Tawala wa Mkoa huo, Ngollo Malenya Mkuu wa Wilaya ya Ulanga na Hanji Godigodi Mkuu wa Wilaya ya Kilombero
Akibainisha zaidi Fatma Mwassa amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 walimu 1800 walipandishwa madaraja huku jumla ya vyumba vya madarasa 908 vyenye thamani ya shilingi 19Bil. vimejengwa kupitia fedha za UVIKO 19.
Aidha, amesema Serikali ya awamu ya sita imejenga jumla ya shule mpya za Sekondari 13 na kugharimu jumla ya shilingi 4.7Bil. Pamoja na mabweni 4 kwa gharama ya shilingi milioni 320. Pamoja na miundombinu hiyo bado amesema Serikali hiyo imetoa shilingi 14.1Bil kwa ajili ya Elimu bila malipo kwa kipindi hicho mwaka 2021/2022 pekee.
Kulia ni Jabiri Makame Mkuu wa Wilaya ya Gairo akipokea mojawapo ya vitabu vya miongozo mara baada ya Mkuu wa Mkoa kuzindua vitabu hivyo kwa nghazi ya Mkoa
Kwa upande wa mafunzo kwa Walimu Fatma Mwassa amesema katika kipindi hicho jumla ya walimu 1853 wamepata mafunzo kazini, mafunzo ambayo ni endelevu na kutumia fursa hiyo kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Morogoro Kumpongeza Mhe. Samia suluhu Hassan kwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali yake.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Hanji Godigodi akikabidhiwa kitabu cha mwongozo huku Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando (katikati) akishuhudia
Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pscal Kihanga naye aliamua kuchukua kitabu hicho ili kujifunza yaliyomo humo ambapo pia kitamsaidia kufanya ufuatiliaji kwa watendaji wake
Katika hatua nyingine Fatma Mwassa amesema, Elimu ni haki ya kila mtoto, kwa sababu hiyo amewaagiza Viongozi ndani ya Mkoa huo hususan walimu, kuhakikisha wanaandikisha kila mtoto pindi muda huo utakapofika huku akisisitiza watoto kutoka Jamii ya Wafugaji kutoachwa hata mmoja.
“sasa niwakumbushe tu kwamba Elimu ni haki ya kila mtoto, hata yule ambaye amezaliwa, wazazi wake hawajatilia umuhim wa Elimu sisi viongozi wa Serikali mkiwemo ninyi walimu mnawajibika kuhakikisha watoto wote wanapata Elimu, na hasa ukizingatia kuwa Elimu ni bure kuanzia Msingi Mpaka Sekondari, kwa hiyo tunavoandikisha tusiziache kando jamii za wafugaji” ameagiza Fatma Mwassa.
Katibu Tawala Msaidizi kwa upande wa Elimu ambaye pia ni Afisa Elimu wa Mkoa huo Bi.Germana Mung'aho (kushoto) akieleza machache kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa (hayupo pichani) kuzindua vitabu hivyo
Pamoja na maagizo hayo Fatma Mwassa amewataka Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo kutoa ushirtikiano wa kutosha katika ngazi ya shule, Kata na Wilaya kuhakikisha walimu wanafanya kazi zao ipasavyo lakini pia wanafunzi wanafundishwa vizuri na kufaulu mitihani yao na kusimamia miongozo iliyoko kwenye vitabu hivyo ili Mkoa uweze kupiga hatua mbele katika Sekta hiyo ya elimu.
Sehemu ya Wadau wa Kikao hicho
Akitoa utangulizi wa kikao hicho cha wadau wa Elimu ngazi ya Mkoa, Afisa Elimu Mkoa wa Morooro Germana Mung’aho amesema, miongozo hiyo mitatu inakwenda kuleta mabadiliko makubwa sana katika sekta ya Elimu na kuwa nyezo muhimu kwa walimu katika kufanyia kazi ili kuboresha elimu ndani ya Mkoa huo.
Akitoa neno la shukrani kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya wa Mkoa huo, amesema wameyapokea maagizo yaliyotolewa na kiongozi wao bila kusita na wako timamu kuyatekeleza kwa kasi inayotegemewa na kiongozi wao.
wadau mbalimbali wa Elimu wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa
Baadhi ya wadau wa kikao hicho hususan walimu, wao pamoja na kushukuru ujio wa miongozo hiyo bado wanashauri kuwepo jitihada zaidi za kuongeza walimu wa masomo ya Sayansi, kwa kuwa wamesema shule nyingi zina wanafunzi hadi 600 lakini mwalimu wa somo la Hisabati au fizikia ama baolojia anakuwepo mwalimu mmoja jambo ambalo wanadai ni ngumu kwa mwanafunzi kuelewa masomo hayo.
Afisa Elimu Msingi kutoka Halmashauri ya Mlimba Wilaya ya Kilombero Witness Kimoleta amesema ili kupata matokeo mazuri kwenye mitihani, Mkoa hauna budi kuwekeza katika ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi za chini ikiwa ni pamoja na kuwa na mitihani ya mara kwa mara, kufanya Tathmini na ufuatiliaji wa kutosha.
Bi. Witness Kimoleta
Naye Mkuu wa shule ya Sekondari Vigoi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Mkoani humo, katika kuboresha Elimu anashauri maeneo mawili yasimamiwe kikamilifu katika ufuatiliaji wa wanafunzi ili kupunguza utoro, lakini pia kufuatilia kwa karibu wanafunzi kupata chakula cha mchana na wazazi ambao hawatekelezi maamuzi hayo itafutwe mbinu ya kutatua changamoto hiyo.
Uzinduzi wa vitabu hivyo vya miongozo ngazi ya Taifa ulifanyika Mkoani Tabora Agosti 4 mwaka huu na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa ufunguzi wa michezo ya UMITASHUMTA NA UMISETA, mojawapo ya miongozo hoyo ni “Mkakati wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji ngazi ya Elimu Msingi”.
Miongozo mingine ni pamoja na “Changamoto katika uboreshaji wa Elimu ya Msingi na Sekondari, nini kifanyike?” na “Mwongozo wa Uteuzi wa Viongozi wa Elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mikoa”.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.