RC Morogoro, atamani Morogoro iwe safi
USAFI WA MAZINGIRA NI JUKUMU LETU SOTE, MIFUMO IFANYE KAZI – FATMA MWASSA
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Aboubakar Mwassa amesema anatamani mazingira ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro yawe safi ili kuepusha magonjwa ya mlipuko na kuipunguzia Serikali mzigo katika kupambana na maadui watatu ambao ni Ujinga, maradhi na umaskini.
Fatma Mwasa ametoa kauli hiyo Septemba 10 mwaka huu wakati akizindua Kampeni ya usafi wa Mazingira katika halmashauri yua Manispaa hiyo alipoungana na wananchi wengine kufanya usafi wa mazingira katika Kata za Mji Mkuu, Sultani area pamoja na mitaa mingine ya mji huo na kutoa maagizo ya Serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa (aliyevaa kofia pana) akifanya usafi wa Mazingira katika kata ya Sultani area, Septemba 10 mwaka huu
Fatma Mwassa ambaye katika uzinduzi huo amekuja na Kaulimbiu inayosema USAFI NI JUKUMU LETU SOTE, MIFUMO IFANYE KAZI, amesema nia yake kubwa ni kutaka Manispaa hiyo iwe safi huku akiagiza Mifumo ya Kiserikali yote kwa maana ya Ofisi au Watendaji wake kuwajibika kufanya kazi hiyo bila kusukumwa.
“Langu ni moja tu, kwamba lazima Morogoro iwe safi, lazima tutunze mazingira Morogoro, tumeanza na kampeni ya usafi kusafisha mazingira lakini kampeni inayuofuata ni ya kupanda miti kila nyumba, na miti hiyo itakuwa ni angalau ya matunda” ameagiza Fatma Mwassa.
Maelekezo mengine ya Kiserikali ambayo yametolewa na kiongozi huyo ni pamoja na kila mwananchi kufanya usafi wa mazingira katika mazingira yanayomzunguka kila siku, na siku ya Jumamosi usafi huo utafanywa kwa pamoja kwa kila mtaa kuanzia asubuhi hadi saa nne na maduka au biashara zitafunguliwa baada ya usafi huo kufanyika.
Aidha, ameagiza kuwa kila Jumamosi ya kwanza ya mwezi kutakuwa na usafi mkubwa utakaoambatana na ukaguzi na kulipa faini kwa wale ambao hawatawajibika kufanya usafi katika maeneo yao huku akiwatahadharisha wananchi kutii sheria bila shuruti na kwamba sheria ndogo zinazohusu usafi wa mazingira kama zilikuwa hazitumiki zianze kufanya kazi yaani kulipa faini ya shilingi 50,000/= kila kosa moja la aina hiyo.
Katika Hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewageukia watendaji wa Serikali wakiwemo Watendaji wa Kata na maafisa Afya ambao hawatasimamia ipasavyo Usafi wa Mazingira katika maeneo yao ya kazi watapewa onyo au kuchukuliwa hatua za kinidhamu kama hawatarekebisha utendaji wao wa kazi hata baada ya kuonywa.
Kwa maneno mengine Mkuu huyo wa Mkoa katika uzinduzi huo hakuridhika na usafi wa mazingira ya Manispaa ya Morogoro, kwa sababu hiyo kazi hiyo ameiacha mikononi mwa Watendaji wa Serikali wakiwemo Watendaji wa Mitaa, Kata, Afya na kuwataka kila mmoja katika ngazi yake na eneo lake atomize wajibu wake kwa kutumia neno fupi tu, MIFUMO IFANYE KAZI.
“usafi wa mazingira ni jukumu letu sote, mifumo ifanye kazi”
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.