Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ametatua mgogoro wa Ardhi uliokuwepo baina ya Halmashauri mbili za Mvomero na Morogoro vijijini uliodumu zaidi ya miaka nane bila ya kupatiwa ufumbuzi.
Mgogoro huo umetatuliwa April 12, 2021 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri hizo, ambapo alifika eneo la tukio katika kijiji cha Mkono wa mara kisha kuzungumza na wananchi juu ya muafaka wa mgogoro huo.
Loata Sanare amebainisha kuwa mgogoro huo ulitatuliwa kwa kukaa mezani kuzugumzia suala hilo, kuunda kamati ya kupima na kugawa ardhi zoezi lililoongozwa na Kamishna wa ardhi Kanda ya Mashariki pamoja na Maafisa Ardhi wa Halmashauri zote mbili, Serikali za vijiji na Wakuu wa Wilaya za Mvomero na Morogoro.
‘’…..narudia kusema nawashukuru sana kamati hii ya ardhi, kwamba mlitumwa kutatua kero za wananchi, kero ambayo miaka mingi imeshindikana, tumekuja tumefanya vikao viwili mgogoro umeisha, lakini narudia kusema mgogoro umeisha kwa maana ya kuoneshana mipaka…..’’ amesema Loata Sanare.
Aidha, Loata Sanare amezitaka Halmashauri hizo baada ya kutambua mipaka yao kutenga Ardhi, kwa ajili ya huduma za jamii ikiwemo Shule, Afya, sehemu za kuzikia, michezo sehemu za kufanyia ibada n.k.
Sambamba na hayo, Loata Sanare ametoa onyo kwa wananchi wanaojimilikisha na kuuza ardhi nje ya taratibu zilizowekwa na Serikali na kuwataka kufuata sheria ili kuepukana na changamoto zinazoweza kujitokeza.
Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi wa Mkoa wa Morogoro Ndg. Frank Minzikuntwe amekiri kuwa Mkuu wa Mkoa amemaliza mgogoro huo wa ardhi uliokuwepo baina ya Halmashauri za wilaya ya Mvomero na Morogoro kutokana na vikao walivyokaa kisha kuweka mipaka ili kila Halmashauri kutambua eneo lake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa Halmashauri hizo akiwemo Bw, Anthony Hoza Mkazi wa Mkono wa mara, ametoa pongezi kwa Mkuu wa Mkoa huyo kwa kutatua mgogoro huo uliokuwa ukitishia Amani kutokana na baadhi ya watu kujimilikisha ardhi kiholela.
Kamishna wa Ardhi wa Mkoa wa Morogoro Ndg. Frank Minzikuntwe akitoa akifafanua namna ambavyo kamati aliyoiunda Mkuu wa Mkoa ilivyotatua mgogoro wa ardhi baina ya Halmashauri hizo
Naye, Fatma Athumani amesema mgogoro huo ulikuwa unamkosesha amani kutokana na uvamizi wa ardhi uliokuwepo ambao ulikuwa unapelekea ugomvi baina ya pande hizo mbili kwa maana ya wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na wale wa Halmashauri ya Morogoro.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.