RC Shigela aagiza kuukarabati mnara wa mashujaa
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameielekeza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuukarabati mnara wa Mashujaa uliopo katika Halmashauri hiyo uweze kufanana na kumbukumbu ya historia ya Mashujaa waliopigania uhuru katika nchi hii.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ( wa kwanza kushoto) akiwa pamoja na kamati ya ulinzi na usalama wakati wa maadhimisho ya siku ya mashujaa ambayo yamefanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Julai 25 mwaka huu.
Shigela ametoa agizo hilo Julai 25 mwaka huu wakati wa maadhimisho ya siku ya Mashujaa yaliyofanyika eneo la Mnara wa mashujaa uliopo eneo la Posta katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kuwakumbuka mashujaa hao waliopambana wakati wa harakati za ukombozi wa Taifa la Tanzania na Afrika kwa jumla.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akielekeza Mnara huo kufanyiwa ukarabati wa haraka
Martine Shigela amesema kuwa Historia ya Mashujaa waliopigania uhuru wa nchi ya Tanzania ni muhimu kutunzwa na kuhifadhiwa vema ili vizazi vijavyo viweze kujifunza na kuelewa vema historia ya Taifa na bara la Afrika.
“Nielekeze kuanza mara moja harakati za kuukarabati Mnara huu kwa kuupaka rangi, kuweka vema Majina ya Mashujaa na kuwasha taa juu ya kilele cha mnara huu ili kuwaenzi mashujaa wetu” ameagiza Shigela.
Aidha, Martine Shigela amesema suala la uzalendo na ushujaa kila mmoja anaweza kulionesha kwa namna yake kulingana na sehemu yake ya kuwajibika ili kuendelea kuitunza amani iliyopo, pamoja na kuliletea maendeleo taifa la Tanzaia.
Baadhi ya wafanyakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro pamoja na wananchi wa Halmashauri hiyo wakifanya usafi katika Mnara wa Mashujaa kama sehemu ya kuwakumbuka Mashujaa hao leo Julai 25 mwaka huu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando amekitaka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kuendeleza vema maeneo na kufufua viwanda ambavyo viliachwa katika Tawi la Chuo hicho lililopo Mazimbu ili kuwaenzi Mashujaa hao kwa kufanya kazi za maendeleo ya kijamii.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando akiweka shada la maua katika mnara huo wakati wa Maadhimisho hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro akiweka shada la maua kama ishara ya kuwakumbuka Mashujaa.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Fortunatus Musilimu ambaye ni Kamanda wa Jeshi hilo Mkoani Morogoro akiwakilisha Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa huo kuweka shada la maua katika Mnara wa Kumbukumbu ya Mashujaa.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe. Pascal Kihanga amebainisha kuwa wamepokea maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kwamba ukarabati wa Mnara huo utafanyika mara moja kwa lengo la kuwaheshimisha Mashujaa hao.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga akiahidi kupokea na kuyafanyia kazi maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kuyatekeleza kwa wakati.
Siku ya Mashujaa huazdhimishwa hapa nchini kila mwaka ifikapo Julai 25 ili kuwakumbuka mashujaa hao walipigania ukombozi wa Taifa la Tanzania na Afrika kwa ujumla, ambapo kwa mwaka huu, maadhimisho hayo kitaifa yamefanyika Mkoani Dodoma katika viwanja vya Mashujaa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.