RC SHIGELA AIAGIZA MORUWASA KUFIKISHA MAJI MKUNDI.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameiagiza Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoani Morogoro (MORUWASA) kuhakikisha inafikisha huduma ya maji katika Kata ya Mkundi iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kabla au ifikapo mwezi Oktoba Mwaka huu ili Wananchi waweze kuondokana na kero hiyo ambayo imewakabili kwa muda mrefu.
Mkuu a Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akitoa ufafanuzi wa kero mbalimbali za wananchi wa kata ya Mkundi Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mei i 31 mwaka huu alipofanya ziara yake ya Kikazi katika Kata hiyo.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa agizo hilo Mei 31 Mwaka huu wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo na kutatua kero za wananchi ambapo amesisitiza kuwa huduma hiyo ni muhimu na tayari Serikali imetenga zaidi ya shilingi 1 Bil. Kwa ajili ya kujenga miundombinu ya maji katika Kata hiyo ya Mkundi.
Martine Shigela amefafanua matumizi ya fedha hizo kuwa zitatumika katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa wa maji likiwemo tenki kubwa linalojengwa maeneo ya Mguru wa ndege kwa gharama ya shilingi 600 mil., Kituo kikubwa cha kusukuma maji kitakachogharimu shilingi milioni 460 ambapo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 98 pamoja na Mtandao wa kusambaza maji utakaogharimu shilingi 600 Mil.
“Nielekeze kwa mtaalamu wetu wa Moruwasa kuhakikisha ahadi zote za maji zinatekelezwa, sitaki kuona maji yanaendelea kukaa kwenye matenki bali nataka kuona maji yanakwenda kwa wananchi ili wananchi waanze kunufaika na huduma hiyo” ameelekeza Shigela.
Katika hatua nyingine Martine Shigela ameagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kufika katika kata hiyo ya Mkundi na kutatua changamoto ya miundombinu ya barabara yakiwemo makorongo ambayo hujaa maji kipindi cha masika na kuwa tishio kwa wananfunzi wa shule za msingi.
Katika kutatua kero hiyo, Mbunge wa jimbo la Morooro Mjini Mhe. Abdulazizi Mohamed Abood ameahidi kutoa kiasi cha shilingi 2.5 Mil, Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela nae ameahidi kuchangia Shilingi milioni moja na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro nayo imeahidi kutoa Shilingi 1.5 Mil. na kufanya Jumla ya fedha zote zilizoahidiwa ambazo zitatumika katika ukarabati wa barabara za ndani ya Kata hiyo kufikia shilingi 5 Mil.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albart Msando ameweka wazi kuwa ipo changamoto ya baadhi ya wananchi wa maeneo ya Mkundi kuvamia hifadhi ya Barabara Kuu ya Dar es Salaam kwenda Dodoma na kujenga majengo ya kudumu na kwamba Serikali ilishatoa katazo la kutovamia hifadhi hiyo lakini wananchi wamekuwa wakikaidi huku akitoa rai kwa wananchi hao kuitikia wito huo vinginevyo Serikali itachukua hatua ya kubomoa majengo yote yaliyojengwa ndani ya hifadhi hiyo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo Bw. Seif Chomoka amewasilisha changamoto za Kata yake zikiwemo miundombinu mibovu ya barabara, ukosefu wa huduma ya maji, ukosefu wa huduma za Afya, uhaba wa madarasa katika baadhi ya shule na changamoto ya soko, changamoto ambazo tayari Mkuu wa Mkoa alizitolea maelekezo kwa wahusika ili kuzitatua haraka.
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga akieleza namna wanavyoshughulikia changamoto za wananchi wa Kata ya Mkundi wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro iliyofanyika Mei 31 mwaka huu katika Kata hiyo.
Nao wananchi wa Kata hiyo ya Mkundi akiwemo Bw. Teresphory Nemes amesema kuwa changamoto ya huduma ya maji katika eneo hilo imekuwa kero kubwa hasa kwa wakazi wa mitaa ya CCT, Ngerengere, Kipera na Kiegea A na B ambapo wanalazimika kununua dumu moja kwa shilingi 500 hadi shilingi 1000.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Mkundi wakisikiliza na kutoa changamoto mbalimbali zinazowakabili maisha yao ya kila siku ikiwemo uhaba wa maji safi na salama.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.