RC Shigela azindua ujenzi wa jengo la Dharura Malinyi, asema hana mgogoro nao, ataka viongozi kushikamana.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigella amezindua ujenzi wa jengo la dharura litakaloghalimu shilingi milioni 390 katika hospitali ya wilaya ya Malinyi ikiwa ni mwendelezo wa ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo huku akipongeza mabadiliko ya kiutendaji yaliyopo sasa na kutaka waendelee kushikamana.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akikagua ujenzi wa majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Malinyi Machi 5 mwaka huu.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni akiwa Wilayani humo katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo yanayojengwa baada ya kupokea fedha shilingi milioni 500 kkutoka kwa Serikalini na milioni 390 kwa ajili ya jengo la Dharura ambalo ujenzi wake umezinduliwa na Mkuu wa Mkoa siku alipotembelea.
Akiwa katika eneo hilo Martine Shigela alikagua ujenzi wa jengo la mionzi, maabara, jengo la kufulia nguo, utawala, jengo la kutolea dawa pamoja na majengo mengine na kuridhika na meandeleo ya ujenzi unavyoendelea na kumpongeza Mkuu wa wilaya Mathayo Masele pamoja na Mkurugenzi Joanfaith Kataraia kwa niaba ya viongozi wengine kwa kusimamia vyema ujenzi huo.
Amesema, kwa sasa hana mgogoro na Viongozi wa Wilaya hiyo kwa kuwa wanafanya kazi kwa weledi, Mshikamano, ushirikiano na umoja huku akiwataka kuendeleza hayo na hasa kusikiliza kero za wananchi waliopo katika Wilaya yao.
“kwa hiyo nataka niwasihi tena sina mgogoro na Malinyi sasa, mkiona nimekuja hapa kueni na Amani chapeni kaz, mkiona kiongozi mkubwa amekuja mimi nitawasemea vizuri mimi Mkuu wa MKoa” amesisitiza Martine Shigela.
Akimkaribisha kuzungumza na wananchi waliojitokeza katika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya hiyo Mathayo Masele amesema pamoja na changamoto chache ambazo bado zipo, changamoto hizo hazitawazuia kuwatumikia wananchi kwa kuwa hizo hazitakuwa dawa ya malaria au kero nyingine walizonazo wananchi wa Malinyi huku Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Joanfaith Kataraia pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuwapelekea shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi Hospitali na milioni 390 jengo la dharura,ameahidi mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa Halmashauri hiyo kamwe haitokuwa tena na historia ya kutomaliza miradi ya maendeleo.
Kwa upande wao wananchi wa Malinyi Asha msenga na Eleonara Mlombole wamempongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea Hospitali ya Wilaya ambayo imeondoa kero walizokuwa wanazipata kutoka Hospitali za Binafsi ikiwemo kubaki Hospitalini endapo hujamaliza kulipa deni la matibabu hata kama umepona suala ambalo kwao lilikuwa kero kwao.
Pamoja na shukrani hizo wamemuomba Mhe. Samia Suluhu Hassan kukamilisha majengo ambayo hayajakamilika yakiwemo nyumba ya kujifungulia waja wazito, Mochwari, jengo la dharura na jengo la kulala wanaotunza wagonjwa kwani kutokuwepo majengo hayo kunapelekea adha kwao.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.