RC SHIGELA AMSHUKURU RAIS KWA KUDUMISHA AMANI, UMOJA
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kudumisha Amani na Umoj wa Taifa hilo huku akibanisha kuwa kwa kipindi kifupi cha siku 365 ameuonesha Ulimwengu kuwa Tanzania ni nchi inayoendesha siasa za kistaarabu.
Umati wa wananchi walioshiriki sherehe za mwaka mmoja wa Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa madarakani, uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (wa pili kushoto) na Katibu wa Chama cha Mapinduzi (wa pili kulia) wakiingia Uwanja wa Jamhuri wakati wa maadhimisho hayo
Martine Shigela ametoa pongezi na shukrani hizo Machi 19 mwaka huu wakati wa sherehe za maadhimisho ya Mwaka mmoja tangu alipoaapa kuwa Rais wa Tanzania sherehe ambazo kimkoa zimefanyika Uwanja wa Jamhuri uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema, tangu Mhe. Samia Suluhu Hassan ashike kijiti hicho cha kuliongoza Taifa la Tanzania yapo mambo makubwa yamefanyika ndani ya kipindi kifupi ikiwa ni pamoja na kuudhihirishia Umma wa Tanzania na Dunia kwa jumla namna Taifa la Tanzania limeendelea kuwa Taifa lenye Umoja, Amani, Mshikamano na Upendo, na kuonesha ukomavu wa Kidemokrasia kwa kuwasamehe baadhi ya Watanzania waliokuwa wamewekwa vizuizini kwa makosa mbalimbali.
Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro akiteta jambo na Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Morogoro Mhe. Dorothy John (kulia)
“Rais wetu ameudhihirishia Umma wa Watanzania na Dunia kwamba Taifa letu limeendelea kuwa Taifa lenye Umoja, Mshikamano, Amani na Upendo, kazi hii ameifanya vizuri, ameonesha Ukomavu wa Kidemokrasia hata wale ambao wamewekwa ndani amekwenda kuwasamehe” amesema Martine Shigela.
Ameongeza kuwa, Baadhi ya Nchi kiongozi mmoja anapomaliza muda wa uongozi wake au kufariki wananchi wake huingia kwenye matatizo makubwa kwa sababu ya baadhi ya viongozi kugombania madaraka hali ambayo hata hupelekea umwagaji damu, tofauti na demokrasia na siasa za Tanzania huku akitolea mfano wa tukio la kifo cha Rais John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021 tukio ambalo limepita kwa amani na utulivu.
Akizungumzia mafanikio ya Mhe. Samia Suluhu Hassan yaliyopatikana katika kipindi chake amesema Mkoa wa Morogoro yapo mengi yaliyofanyika ikiwa ni pamoja na kupokea zaidi Shilingi Billioni 11 fedha za Elimu bila Malipo.
Aidha, amebainisha kuwa shilingi Bilioni 30 zimetolewa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Miundombinu ya Elimu ambapo zaidi ya Maboma 302 yamekamilishwa na Madarasa 849 yamejengwa kwa kutumia pesa za Uviko 19.
Pamoja na mafanikio hayo amesema bado Serikali hiyo ilitoa shilingi Bilioni 19, ndani ya Mwaka mmoja huo huo na kujenga Shule Mpya 23 kama sehemu ya kuinua Elimu ya ngazi mbalimbali ndani ya Mkoa huo.
Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa, katika Sekta ya Afya ndani kwa kipindi cha mwaka mmoja cha Mhe. Samia Suluhu Hassan amejenga zaidi ya zahanati 29 kwa gharama ya shilingi Bil. 42, huku Sekta ya Maji ikipewa zaidi ya shilingi bilioni 186 ambapo Mkandarasi yupo mbioni kuanza kazi za ujenzi wa kuwapatia wananchi wake maji safi, salama na tosherevu.
Kuhusu umeme Vijijini Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza Wakuu wa Wilaya pamoja na Viongozi ngazi ya Kata kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa zaidi ya bilioni 52 zilizoletwa na Mhe. Rais Samia kwa ajili ya kufikisha nishati ya umeme zaidi ya vijiji 260.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Morogoro Bi. Doroth Mwamsiku amesema, Chama kupitia ngazi zake za Tawi, Kata, Wilaya na Mkoa wamesimamia Miradi yote iliyotajwa na kuwahakikishia Wananchi kwamba miradi hiyo imekamilika kwa ufanisi mkubwa na kwa kiwango cha hali ya juu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro Mhe. Dorothy John
Wakizungumza katika sherehe hizo kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya wengine, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Majid Mwanga wamesema Mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan umekuwa ni mwaka wa mafanikio makubwa na umefungua na kurahisisha shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hizo.
Mkuu wa WilayayaMorogoro Albert Msando
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Majid Mwanga
Akitoa salamu za shukrani Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga amesema kuwa, Manispaa ya Morogoro inamshukuru Mhe. Rais Samia kwa kufanikisha Shughuli mbalimbali za Miradi ya Maendeleo ikiwa ni pmoja na kufanikisha Mkopo wa Shilingi bilioni 1 kwa ajili ya shughuli za Mipango Miji zitakazotumika katika Upimaji wa Viwanja zaidi ya 1,500 ndani ya Manispaa hiyo.
Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.