Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amepiga marufuku kwa wafanya biasha Mkoani humo kuongeza bei ya vyakula hususan mchele na mafuta ya kupikia kwa kuwa amesema hakuna sababu yoyote inayowafnya wafanya biashara hao kuongeza bei wakati huu ambapo waumini wengine wako katika kipindi cha Mfungo wa Ramadhani na wengine kwenye mfungo wa Kwaresma.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (kulia) akipokea na kutatua kero za Wafanyabiashara wa Soko la Mawenzi Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro
Martine Shigela ameyasema hayo Aprili 13 Mwaka huu alipofanya ziara ya kushtukiza katika Soko Kuu la Chifu Kingalu na Soko la Mawenzi yote ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kudhibiti mfumuko wa bei ya vyakala na bidhaa nyingine ili kupunguza makali ya maisha hususan katika kipindi hiki cha Mfungo wa Ramadhan na mfungo wa Kwaresma.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema haipendezi na ni dhambi kwa mfanyabiashara yeyote atakayeongeza bei ya bidhaa hizo bila kuwa na sababu msingi isipokuwa kwa lengo la kutengeneza faida huku akijua kuwa kuna watu wako katika mfungo na wanahitaji bidhaa hizo kuliko wakati mwingine.
“kwa hiyo tusitemngeneze faida kwenye matatizo ya wananchi, tusitengeneze faida wakati wako kwenye toba, tusitengeneze faida wakati watu wamefunga wakimlilia Mungu mvua inyeshe watu waongeze uzalishaji” amesema Martine Shigela.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amezitaka mamlaka zinazosimamia soko la Mawenzi kuhakikisha zinaratibu mfumo utakaowezesha wafanya biashara wa soko hilo wanaofanya biashara zao nje ya soko kufanyia biashara zao ndani ya soko kwa lengo la kukuza Mapato ya Halmashauri na kuleta usawa baina yao na wafanyabiashara wa ndani ya soko hilo.
Katika hatua nyingine Martine Shigela ameiagiza Halmashauri hiyo kufanya maboresho madogo ya Soko hilo la Mawenzi ili kuondoa adha iliyopo sasa ya kukosa sakafu kutoezekwa hivy kusababisha tope wakati wa mvua na kupigwa na jua.
Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi. Halima Okash ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomerlo amewataka wafanya biashara wa soko la Mawenzi kutokubali kugawanyika kwa sababu yoyote ile bali waungane na kutoa kero zao kwa viongozi kupitia utaratibu uliopo.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Halima Okash akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Mawenzi
Kwa upande wake Meya ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Paschal Kihanga amesema soko la Mawenzi kwa sasa lina changamoto lukuki. Hata hivyo amesema wanaotakiwa kuboresha ni wafanyabiashara wenyewe kupitia makusanyo ya kodi ya pango ili kutekeleza hilo lazima wafanya biashara wote kujenga tabuia ya kulipa kodi ya pango na ili kulipa kodi ya pango wanatakiwa wafanye biashara zao ndani ya soko na sio nje ya soko.
Kulia ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga
Pamoja na ushauri huo Mstahiki Meya ameto ushauri kwa uongozi wa Mkoa wa kutaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashaufri ya Manispaa ya Morogoro kuruhusiwa kutumia mgambo katika kusaidia shughuli za ulinzi wa soko la Mawenzi ikiwa ni pamoja na kutoruhusu wafanyabiashara kufanya biashara zao nje ya soko hilo.
Sambamba na Meya wa Manispaa hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ya Manispaa ya Morogoro ndugu Ally Machela amesema, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro katika bajeti ijayo ya 2022/2023 imetenga Tsh Milioni 350 ili kufanya ukarabati mkubwa katika Soko hilo lengo ni kuhakikisha wafanya biashara wanafanyabiashara zao katika mazingira safi na yaliyo salama.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Ally Machela (wa nne kushoto)
Meneja wa Soko la Mawenzi Bw. Abdully Mkangwa amesema malalamiko ya wafanyabiashara kuuzia biashara zao nje ya Soko ni sahihi lakini changamoto ni kuwa wapo baadhi ya wapangaji wa Meza za kufanyia biashara hawalipi kodi kwa usahihi kutokana na kuwa baada ya kupanga nao hupangisha watu wengine hali inayopelekea ugumu wakati wa kukusanya kodi ya pango na wanapojaribu kufuatilia kwa karibu kwa kuwafungia vizimba hadi watakapokuwa wamelipa hupewa kesi za kuharibu mali za watu.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.