Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewapongeza Wanakikundi cha Jamii Mpya Tanzania kwa uamizi wao wa kufanya Utalii wa ndani Katika Mbuga ya wanyama ya Mikumi ishara ya kuunga mkono jitihada za Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza Vivutio vya Utalii wa nchi kupitia Filamu ya Royal Tour.
Martine Shigela ametoa pongezi hizo leo Mei 14 wakati wa ziara yake ya kuwatembelea Watanzania zaidi ya 1000 kutoka Mikoa mitatu ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam waliotembelea Mbuga ya Mikumi kama sehemu ya kutoa hamasa kwa wananchi wengine kuweza kufanya utalii wa ndani ili kuchangia pato la taifa na kukuza uchumi wa taifa.
Aidha, Martine Shigela amebainisha kuwa, kuamua kuunga mkono jitihada za Rais kwa vitendo kutatoa sura mpya kwa vijana na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kujiajili na kuweza kuendesha Maisha kwa kujipatia kipato kwa kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo hasa kwa jamii iliyo karibu na maeneo husika ya Utalii.
“Wapo Tourguide hapa wanaojitolea na wamesomea ambao hawaajiliwi na Serikali lakini wanaijua sana Mbuga na wananaweza kukuelekeza vizuri, ukitaka kumuona simba twende huku.." amesema Shigela.
"akinamama wanaozalisha mbogamboga, mayai, maziwa, matunda na kuku watapata masoko kwa sababu wageni wakija watahitaji chakula” ameongeza Martine Shigela.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amesema biashara yoyote ili iwe na mafanikio ya haraka na ya kweli lazima yawe na matangazo kama ambavyo Mhe. Rasi Samia amefanya kitaifa na kimataifa katika kuitangaza Filamu ya Royal Tour.
Naye Naibu Kamishina wa Uhifadhi kanda ya Mashariki Bi Asteria Ndaga amewapongeza vijana hao kwa kuwa vijana wa kihistoria, kwani tangu kuanzishwa kwa utalii Katika taifa hili vijana hao ndio waliotalii kwa idadi kubwa na kwa mara moja.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mikumi Mhe. Dennis Londo ameweka wazi kuwa kitendo hicho walichofanya vijana hao kitaitangaza Mbuga hiyo ya Mikumi na kusaidia kuleta watalii wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi hivyo kuleta mafanikio makubwa katika taifa kupitia sekta ya utalii.
Zaidi mwenyekiti wa Kikundi cha Jamii Mpya Tanzania Bi. Magdalena Nachunga amesema kwa kuanzia wameanza kutalii Mbuga hiyo ya Mikumi lakini lengo kuu si kuishia hapo bali ni kuzunguka na kutoa hamasa nchini nzima lengo ni kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili utalii uweze kuwanufaisha watanzania wote kikamilifu.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.