Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameziagiza Taasisi za Serikali, Mashirika binafsi pamoja na Taasisi za kidini kushirikiana na kuongeza jitihada za kutokomeza mimba za utotoni Mkoani humo kwa Watoto walio chini ya miaka 21 kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari.
Martine Shigela ametoa agizo hilo Mei 10 Mwaka huu wakati akifungua Mkutano wa kutambulisha Mradi wa Kutokomeza Mimba za Utotoni unaotarajia kuendeshwa na tasisi ya RELIEF TO COMMUNITY DEVELOPMENT ORGANISATION ( RECODO) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo na kushirikisha wadau mbalimbali.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa lazima uwepo ushirikiano baina ya taasisi za kidini, taasisi za Kiserikali, Mashiririka binafsi pamoja wadau wengine wakiwemo wazee wa kimila katika kuhakikisha changamoto ya mimba za utotoni inatokomezwa kabisa Mkoani humo, kwani suala la kupunguza au kutokomeza mimba utotoni ni suala jumuishi na sio suala la Taasisi moja.
“hili si jambo la Recodo peke yao bali ni jambo la jamii kwa ujumla na ndio maana tukashirikisha taasisi nyingi wakiwemo viongozi wetu wa dini ili sasa kuja na paper itakayotuongoza nini kifanyike, nani afanye nini kwa wakati gani. Nadhani tukija na hio paper itatusaidia kuwa na wider platform itakayohusisha viongozi wa Wilaya lakini pia Viongozi mbalimbali watakao kuja kushiriki Kikao chetu”. amesema Martine Shigela.
Katika hatua nyingine, Martine Shigela ameongeza kuwa ili kuhakikisha mtoto wa kike anasaidiwa kufikia malengo yake,a Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imetenga fedha kwa kila jimbo Mkoani humo kwaajili ya kujenga Shule za Sekondari Mahsusi kwa ajili ya kuwasaidia Watoto wa kike ili kutimiza ndoto na malengo yao na sio kukatishwa malengo kwa sababu ya changamoto ya mimba za utotoni.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya RECODO Bwana Saidi Muya ameeleza kuwa kama taasisi wanapokea na kufanyia kazi maagizo ya Mkuu wa Mkoa na kwamba watatanua wigo kwa kushirikiana na wadau wengine sio tu kwa kutokomeza mimba za utotoni bali watapambana pia na masuala ya mapenzi ya jinsia moja kwani nayo ni sababu ya Watoto kuharibika na kuachana na masomo bila kutarajia.
Akiwakilisha vyombo vya ulinzi na usalama Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Fortunatus Muslim amesema kwamba ili RECODO waweze kufanikisha shughuli hiyo ni lazima wapate uzoefu wa ukusanyaji wa data kutoka kwa wadau wazoefu likiwemo Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha dawati la jinsia kwa lengo la kukomesha kabisa masuala ya ubakaji, mimba za utoto na ulawiti hali itakayowezesha Watoto na wanafunzi kutimiza malengo na ndoto zao za kupata Elimu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.