ARC SHIGELA ATAKA KASI UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewaagiza watendaji wa Serikali Mkoani humo kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa, inatekelezwa kwa kasi kubwa na kukamilika kwa wakati huku ikiwa na ubora unalingana na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali.
Shigela ametoa agizo hilo wakati wa hotuba yake ya kufungua Kikao cha Ushauri cha Mkoa kilichofanyik Machi, 9 mwaka huu Cate Hotel iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Amesema Serikali imetoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo watendaji wa idara husika wahakikishe wanawajibika katika kukamilisha miradi hiyo kwa kasi ile ambayo ilitumika wakati wa kutekeleza miradi ya fedha za UVIKO – 19.
Katika hatua nyingine amewataka viongozi wenye dhamana ya kutafuta maeneo kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo mipya kutochukua maeneo yenye migogoro ya Ardhi na kusababisha mradi kuleta kero kwa jamii badala ya mradi huo kuwa neema kwa jamii husika.
“Tuhakikishe kuwa miradi ambayo iko kwenye maeneo yetu tunaifuatilia kwa karibu, tuhakikishe miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango na thamani ya fedha zilizotengwa, tuhakikishe hatutengenezi mkigogoro ya maeneo gani yatumike kwa ujenzi wa hiyo miradi” amebainisha Martine Shigela.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu Mkoa wa Morogoro Anza Amen Ndossa
Akizungumzia migogoro ya ongezeko la mifugo Mkoani humo amependekeza mbinu ya kukabiliana na changamoto hiyo ambapo amezitaka Halmashauri za Wilaya kuangalia uwezekano wa kutengeneza sheria ndogo za kutoza faini wale wote watakaoingiza mifugo yao mkoani humo ikiwa na chapa za mikoa mingine
“sasa labda tutengeneze Bylaws au sheria ndogo kwamba ukienda ku shift bila kibali chochote na nembo yako inaonekana ya Mkoa Fulani basi unapigwa faini kwa sababu utakuwa na wewe kama ni mvamizi kwenye maeneo ambayo hujaruhusiwa kwenda, tukifanya hivyo tunaweza ku control mifugo kwenye maeneo yetu bila shida yoyote” amesema Shigela.
Naye Mbunge wa jimbo la Kilosa Mhe. Prof. Palamagamba Mwaluko Kabudi ameonesha umuhim wa Mkoa wa Morogoro kwa nchi ya Tanzania na namna unavyotegemewa katika kusukuma Uchumi wan chi kwa kuwa Mkoa una ardhi nzuri, miundombinu tosherevu, hali ya hewa inayokubalika kwa kilimo cha mazao karibu yote na kwamba umejaliwa kuwa na madini, vyanzo vya maji ya kuzalisha Umeme pamoja na viwanda vya Sukari.
“Kama upo Mkoa Tanzania namba moja katika kuifanya nchi hii ibadilike na iwe na maendeleo ya juu, Mkoa huo ni Morogoro. Lakini sina hakika mimi na ninyi kama tunajua dhima maalum ya Mkoa wa Morogoro katika kupelekea maendeleo ya nchi hii kwa kasi zaidi” amebainisha Prof. Kabudi.
Prof. Kabudi ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Rais, ya Utawala na Serikali za Mitaa, akichangia hoja za kikao hicho amewafunda watumishi wa umma kutofanya kazi kwa ajili ya vyeo bali kutekeleza majukumu waliyopewa na kutaka matokeo bora yanayoweka historia kwao na vizazi vijavyo.
Kwa mujibu wa muwasilishaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 ya Mkoa wa Morogoro Mchumi Emmanuel Mazengo amesema Mkoa umewasilisha makisio ya fedha jumla ya shilingi 411.72Bil. kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo, kiasi hicho kimeongezeka kwa 12% ukilinganisha na bajeti inayoendelea sasa.
Aidha Mchumi huyo amewaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa kwa bajeti ya mwaka 2020/2021 hadi Disemba 2021 jumla ya shilingi Bil. 192.14 sawa na 52% zilikuwa zimekwishatumika.
Akifafanua matumizi ya fedha za UVIKO- 19 shilingi 20.25 ambazo Mkoa ulizipokea amesema fedha hizo zilielekezwa katika miradi ya Elimu na Afya,
Ambapo amesema hadi Disemba 2021 madarasa 707 ya shule za Sekondari yalikuwa yamekamilika na vyumba vya madarasa 142 ya shule shikizi nayo yamekamilika na wanafunzi ambao walikuwa wanapata shida kujifunza sasa wanasoma ndani ya madarasa yenye nafasi.
Aidha, kikao kilielezwa kuwa Mkoa ulipokea fedha kutoka Serikalini jumla ya shilingi 3.19 ni fedha zilizotokana na tozo za mihamala ya simu ambazo zenyewe zimewezesha maboma 35 kujengwa na vituo vya Afya 11 ambavyo vyote viko katika hatua ya mbalimbali za utekelezaji.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.