Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amedhamiria kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa ni Mkoa usio na Migogoro na kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa Watanaznia wengi kuwa Mkoa huo ni Mkoa wa mapigano, vurugu na migogoro baina ya wakulima na wafugaji jambo ambalo amesema kwa sasa linaanza kuwa ni historia.
Shigela ametoa kauli hiyo Juni 21, mwaka huu wakati wa hafla fupi ya uwaapisho wa Wakuu wa Wilaya watano walioteuliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu ndogo Mjini Morogoro huku akiwataka Wakuu hao wa Wilaya kuubrandi Mkoa huo kuwa na TASWIRA nzuri.
RC Martine Shigela akiwa na RAS Bi. Mariam Mtunguja mara baada ya kuapishwa kwa Wakuu wa Wilaya wa Mkoa wa Morogoro.
Shigella amesema Mkoa wa Morogoro ni Mkoa mzuri, una rasilimali nyingi ambazo ni nadra kuzipata katika Mikoa mingine ya nchi hii ikiwa ni pamoja na kuwa na zaidi ya mito mia moja inayotiririsha maji kwa mwaka mzima.
DC Mvomero Halima Okash akisikiliza maelekezo ya RC Shigela.
Rasilimali nyingine alizozitaja zilizopo ndani ya Mkoa huo ni pamoja na uwepo wa maeneo makubwa ya Ardhi, Ardhi yenye rutuba, hali ya hewa safi, pamoja na vivutio mbalimbali vya Utalii ikiwemo maporomoka ya Maji na wanyama pori.
Vingine ni hifadha za misitu, hifadhi ya mazingira asili ambapo vinapatikana vinyonga aina yake wenye pembe tatu wanaopatikana katika milima ya Uluguru, na wanyama aina ya sheshe na panzi wenye rangi ya Bendera ya Taifa letu ambao wote wanapatikana katika bonde la Mto Kilombero pekee. Pia kuna misitu na mbuga za wanyama kama Mikumi, Udzungwa na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
Pamoja na kuzitaja rasilimali na vivutio hivyo kwa uchache, Shigela amesema Mkoa wa Morogoro umekaa kimkakati zaidi kiuchumi katika maana ya upo katikati kimawasiliano ambapo unapitiwa na Reli ya Kati, Reli ya TAZARA, na sasa inajengwa Reli ya Mwendo Kasi – SGR ambayo nayo inakatisha katikati ya Mji wa Morogoro.
Amesema Mkoa huo pia unapitiwa na Barabara kuu iendayo mikoa yote ya nyanda za juu kusini mwa nchi yetu na Mikoa mingi iliyoko kanda ya kati na ile iliyopo Kaskazini mwa nchi hii na nchi nyingine jirani.
Kutokana na uzuri wa rasilimali na fursa hizo, Mhe. shigela amesema kuna haja sana ya kuutangaza Mkoa wa Morogoro na kuyatangaza mazuri hayo yaliyopo ili kufuta dhana ya Watanzania wengi ambao wamezoea kusikia vurugi pekee zinazojitokeza Mkoani humo badala yake wayaone mazuri mengi ambayo yamefichwa na hayo mabaya machache.
‘’Tunayo mengi mazuri tu ya kufanya, tuubrand Mkoa, duniani kote wanabrand mambo mazuri. Hata kama kuna mengine mabaya unasema ili tuangalie namna ya kurekebisha’’ amesema Shigella.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa waandishi wa Habari wanaowakilishi vyombo vyao vya habari Mkoani humo kutoa ushirikiano katika kuutangaza Mkoa huo na kutangaza mambo mema yanayofanyika na yaliyopo ndani ya Mkoa huo huku akiwapongezi kwa kazi nzuri wanazozifanya.
“Tunawajibu wa kuibrandi picha ya morogoro kuwa nzuri, brand yetu siyo nzuri, brand ya Mkoa wa Morogoro ni vurugu, migogoro na ugomvi, ukiona tangazo la Morogoro kwenye TV utegemee mabaya, sasa na nyie waandishi wa habari mpunguze hayo, duniani kote wanabrandi vizuri tu” amesema Shigela.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.