Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewataka Maafisa Elimu Mkoani humo kuweka mpango mkakati wa somo la lishe kufundishwa shuleni ili kutokomeza utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
Shigela ametoa agizo hilo Julai 16 mwaka huu kwenye kikao cha nusu mwaka kilicholenga kutathimini Mkataba wa mpango wa lishe na Bima ya Afya ya jamii iliyoboreshwa yaani iCHFkilichifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Gronency katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Shigela amesema, kufundishwa kwa somo hilo Shuleni kutawasaidia wanafunzi kutambua matumizi Bora na sahihi ya vyakula ambavyo vinatakiwa kuliwa kwa kuzingatia kanuni na miongozo inayotolewa na wataalam wa Afya hivyo kuwajengea Afya nzuri watoto hao.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa huyo amewaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro wakishirikiana na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri wa Mkoa huo kuendelea kuweka jitihada za kutafuta mbinu mbalimbali za kuongeza idadi ya wanachama wa Mfuko wa Bima ya Afya iliyoboreshwa (iCHF).
Sambamba na hilo Shigela amewataka viongozi hao zoezi la kuongeza wanachama liende sambamba na uboreshaji wa huduma za Afya kwa wanachama wake ili wanachama hao waone umaana wa Kujiunga na Mfuko huo na kuondoa malalamiko yanayotolewa na wanachama wake katika maeneo yetu ya kutolea huduma ya Afya kuwa hawapata dawa kupitia Bima hiyo.
‘’Bado Mkoa wetu wa Morogoro tuna changamoto kubwa ya Bima hii ya Afya iliyoboreshwa, asilimia ya wanachama wetu tuliowaandikisha hawapati huduma kama inavyostahili, kumekuwa na malalamiko sana katika upande huu wa Bima, wengi wanalalamika kuwa dawa hakuna wakati sehemu zingine dawa zipo’’ amesema Shigela.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa huo Bi. Mariam Mtunguja amebainisha moja ya changamoto inayokabili Bima ya Mfuko wa iCHF ni kutokuwepo wanachama wa kudumu kutokana na huduma zisizo aminika ambazo hupelekea wanachama hao kutohuhisha bima zao mara tu baada ya kuisha muda wake.
Hata hivyo, Bi. Mtunguja amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmshauri zote za Mkoa huo kuwa mstari wa mbele katika kutoa Elimu juu ya faida mbalimbali ambazo zinatokana na (iCHF) ili kuongeza idadi ya wanachama wa kudumu katika mfuko huo.
Awali akiwasilisha taarifa ya Mfuko wa Bima ya Afya Mratibu wa CHF Mkoa wa Mrogoro Bi. Elicia Mtesigwa amesema bado wanaendelea na uhamasishaji ili kuyafikia makundi mbalimbali ndani ya jamii ili yajiunge na mfuko, huku akieleza lengo lake sio tu kuwa na wanachma wengi bali kuhakikisha kila mwananchi Mkoani humo anakuwa na uhakika wa kupata matibabu ya Afya wakati wote hata anapokuwa hana fedha mkononi.
Pia, Bi. Elicia amebainisha kuwa zaidi ya wanachama 56, 000 Mkoani Morogoro wamejiandikisha katika mfuko wa Bima ya Afya iliyoboreshwa kwa mwaka wa fedha 2020/2021 sawa na asilimia 9.5 ya kaya 590,006 ambapo kaya 21, 941 kati ya hizo zinaweza kupata matibabu katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
Mpango wa Bima ya Afya ya iCHF ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM ndicho kilichounda Serikali iliyopo madarakani, ambapo katika Ibara ya 83 (e) ukurasa wa 186 inazungumzia uimarishaji wa mifuko ya Bima ya Afya nchini ikiwemo NHIF na CHF) ili kufikia lengo la Serikali la kuwa na Bima ya Afya kwa wananchi wote hapa nchini.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.