Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewataka wananchi Mkoani humo kutunza na kusimamia vizuri miradi yote inayotekelezwa na Taasisi ya Kiislam (The Islamic Foundation - TIF) ili kujenga ustawi imara wa jamii ya watanzania.
Shigela ametoa agizo hilo Agosti 31 mwaka huu alipotembelea miradi mbalimbali inayotoa huduma za kijamii katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na taasisi hiyo.
Amesema wananchi wa Mkoa huo wanatakiwa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi hiyo bila malipo yoyote na kuisimamia ipasavyo kwa manufaa ya watanzania kwa jumla.
Aidha, Shigela ametembelea miradi mitano inayosimamiwa na taasisi hiyo ikiwemo Shule ya Sekondari ya Forest, Kituo cha Afya cha Msamvu, Ujenzi wa bomba la maji Shule ya Msingi Msamvu A, Kituo cha watoto yatima na ujenzi wa Msikiti utakaoghalimu zaidi ya Shilingi Bil. 5 za kitanzania,
‘’Natoa pongezi kubwa kwa Mwenyekiti wa The Islamic Foundation, ndugu yangu Aref Nahdi kwa maono chanya aliyonayo kwa wananchi wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla, miradi hii inawajenga kiimani na kiroho katika kuachana na matukio ya kihalifu’’ amesema Shigela.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TIF Aref Nahdi amempongeza Shigela kwa kuitikia wito wa kutembelea miradi hiyo na kumuahidi kuendelea kujenga miradi mingine ya kijamii katika Mkoa wa Morogoro ikiwemo kutoa madawati kwa ajili ya wanafunzi wa Shule ya Msing Msamvu A.
Sambamba na hayo, Nahdi amebainisha kuwa TIF ni taasisi ya kwanza Afrika kwa kufanya vizuri katika utoaji misaada katika jamii na ya tatu ulimwenguni kutokana na ukaribu wanaoujenga baina ya taasisi hiyo na viongozi wa Serikali.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka MORUWASA Victor Ngoyi, ameiomba TIF kuwafikishia maji wananchi sehemu ambazo hawajafika hususan maeneo ya pembezoni ili kuondoa kero ya upatikanaji wa maji wanayoipata wananchi.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.