RC Shigela ataka watanzania kupenda vya kwao,apongeza viwanda vya nguo, mpunga
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewataka watanzania kupenda bidhaa zinazotengenezwa ndani ya nchi ikiwa ni pamoja na bidhaa zinazotengenezwa kwenye viwanda vilivyopo hapa nchini kwani kwa kufanya hivyo licha ya kuendeleza na kudumisha utamaduni wa kitanzani lakini pia tutakuza uchumi wa nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akiangalia na kupongeza wamiliki wa kiwanda cha nguo cha 21st Centuary Ltd kwa kutengeneza nguo na sale za majeshi mbalimbali ya Tanzania kwa ubora wa kimataifa
Martine Shigela ametoa kauli hiyo Novemba 8 mwaka huu alipotembelea kiwanda cha nguo cha 21st Century Textile Ltd na kiwanda cha kuchakata mpunga cha Mw Rice Millers Ltd vilivyopo Mkoani humo huku akiridhishwa na shughuli za uzalishaji zinazofanyika katika viwanda hivyo.
Akibainisha kuhusu kiwanda cha nguo cha 21st Centuary, Mkuu huyo wa Mkoa amesema hakuna sababu ya kwenda kunuua nguo nje ya nchi kwa kuwa nguo zinazozalishwa kwenye kiwanda hicho zina ubora wa kimataifa na kila aina ya nguo inazarishwa kwenye kiwanda hicho.
“lakini kubwa zaidi ni kuwasihi watanzania tupende vitu vya ndani, bidhaa nilizoziona hapa zinakidhi vigezo vya ubora wa kimataifa….kwa hiyo hakuna sababu ya kuagiza nguo kutoka nje. Tuhakikishe tunanunua mali kutoka viwanda vya ndani tukihakikisha mali imeisha ndipo tukatafute viwanda vya nje” ameshauri Martine Shigela
Akiwa katika kiwanda hicho, Shigela amekagua kazi za kutengeneza nguo za aina mbalimbali katika kiwanda hicho zikiwemo sale za wanafunzi, vitenge, mashuka, tisheti, nguo za majeshi mbalimbali ya Tanzania, jezi kwa ajili ya michezo, mablanketi na nguo nyingine.
Mhe. Shigela (kushoto) akiangalia baadhi ya bidhaa (Kanga na Vitenge) zinazozalishwa kiwandani hapo
Aidha, Shigela amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua nafasi ya wawekezaji katika kukuza uchumi wa mtu mmoja na taifa kwa ujumla hivyo wamefanya maamuzi sahihi ya kuwekeza katika kiwanda hicho ambacho kinachangia kukuza uchumi wa taifa.
‘’Morogoro ipo katikati ya makao makuu ya nchi yetu Dodoma lakini pia ipo katikati ya Mji wa kibiashara Dar es salaam, mtu anapowekeza hapa kwanza upatikanaji wa raw material unakuwa ni mwepesi’’ amesema Shigela.
Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho wakiwa kazini wakishona nguo za aina mbalimbali
Sambamba na hayo, shigela ameahidi kuzifanyia kazi changamoto wanazokumbana nazo ikiwa ni pamoja na upungufu wa maji, kukati kwa umeme mara kwa mara au kukata bila kupewa taarifa mapema ili kiwanda hicho kiweze kufanya kazi masaa yote 24.
Hata hivyo amewataka wamiliki wa viwanda hivyo kuzingatia na kutekeleza maelekezo yanayowalinda waajiriwa wakiwa mahali pa kazi ikiwa ni pamoja na kupatiwa vifaa vyote muhimu kwa ajili ya kujikinga na ajali zinazoweza kujitokeza wakiwa kazini, huku akiwataka OSHA kufika katika maeneo hayo kujiridhisha mazingira ya wafanyakazi katika viwanda hivyo.
Awali akibainisha changamoto wanazokumbana nazo katika kiwanda nguo, Afisa Sheria na Utawala Bw. Nicodemas Mwaipungu amesema upungufu wa maji ni kikwazo cha uendeshaji wa shughuli za kiwanda hicho hususan wakati wa kiangazi, uchache wa masoko na kukatika kwa umeme bila taarifa kunapelekea hasara kiwandani hapo.
Hata hivyo, Shigela alihitimisha ziara hiyo kwa kukitembelea kiwanda cha kuchakata mpunga cha Mw Rice Millers Ltd ambapo amemhakikishia mwekezaji wa kiwanda hicho kuwasilisha ombi lao kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassani la kuongezewa eneo la uwekezaji ili mpunga unaozalishwa hapa nchini uchakatwe Mkoani Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (katikati) akiangalia mchele uliokwisha chakatwa, tayari kwa kufungashwa na kusafirishwa nchi za nje
Kwa upande wake Meneja wa Kiwanda cha MW Rice Millers Ltd, licha ya kumshukuru Mkuu wa Mkoa kutembelea kiwandani hapo amewataka watanzania katika mikoa yote kuzalisha mpunga kwa wingi na wao wako tayari kununua ili kuzalisha mchele bora hapa nchini na Africa Mashariki.
Kiwanda cha nguo cha 21st Century Textile Ltd kimebinafsishwa kutoka Serikalini mwaka 2003 kwa sasa kimeajiri ajira za kudumu watu zaidi ya 2,400 na kinanunua pamba kutoka kwa wakulima moja kwa moja zaidi ya tani 600 kwa mwezi hivyo kuondoa tatizo la ajira kwa vijana lakini pia kupunguza changamoto ya wakulima wa zao la pamba kukosa masoko ya kuuzia pamba yao.
Moja ya mitambo inayopatikana kiwandani hapo
Mkuu wa Mkoa Martine Shigela akipewa maelezo namna nyuzi za pamba zilivyotengenezwa
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.