RC shigela asitisha leseni, muda mfupi baada ya kuitoa
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amesitisha leseni ya uchimbaji na ununuzi wa madini muda mfupi baada ya kuitoa kwa kikundi kimoja cha uchimbaji madini ya dhahabu katika kijiji cha Kitaita Wilayani Gairo Mkoani humo baada ya kunusa uwepo wa dhuluma wanaoweza kufanyiwa wachimbaji wadogo wa madini wa eneo hilo.
Martine Shigela amefikia uamuzi huo Mei 26 mwaka huu alipofanya ziara ya kawaida ya kukagua miradi ya maendeleo na kutatua kero za wananchi Wilayani Gairo ambapo alifika pia katika Mgodi wa Madini ulioko katika Kijiji cha Kitaita ili kujionea namna shughuli za uchimbaji wa madini wa eneo hilo unavoendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akiongea na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu (hawapo pichani) katika kijiji cha Kitaita Wilayani Gairo
Katika eneo hilo Mkuu huyo wa Mkoa alipokea changamoto mbalimbali za wachimbaji hao ikiwemo bei ndogo ya ununuzi wa madini pamoja na utata wa asilimia ya viroba vya mchanga wenye madini vinavyotakiwa kuchukuliwa na Kikundi cha madini cha Nguvu moja ambacho kiliomba kumilikishwa sehemu ya ardhi ya mgodi huo wa dhahabu ambacho tayari kilikuwa kimekupewa leseni hiyo na kiongozi huyo muda mfupi baada ya kufika.
Mwenyekiti wa Chama (CCM) Wilaya ya Gairo Shaban Sajilo akiongea na wachimbaji wadogo wa madini
Baadhi ya Viroba vya mchanga wa dhahabu vinavoonekana hapo
RC Shigela akikagua eneo la uchimbaji madini, kushoto kwake ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Ezron Kilamhama
Hii ndo hali halisi ya machimboni
Baada ya Mkuu wa Mkoa kupokea changamoto hiyo na wahusika akiwemo Afisa Madini Wilaya ya Gairo Tito Mahela kushindwa kutoa kwa kina ufafanuzi wa changamoto hiyo, Martine Shigela akalazimika kusitisha matumizi ya leseni aliyokuwa ameitoa muda mfupi kwa kikundi cha nguvu kazi na kwamba uchimbaji huo uendelee kufanyika kama ilivyokuwa awali kabla ya leseni hiyo lutolewa hadi Juni 4 mwaka huu atakapokutana na pande zote zinazohusika akiwemo Afisa Madini Mkoa wa Morogoro ili kulipatia ufumbuzi suala hilo.
“…..suala la mgawanyo baina ya mwenye Leseni na yule asiye na Leseni, jambo hilo nalisitisha mpaka wakalieleze vizuri ofisini” amesema Shigela.
“Tarehe 4 asubuhi nitakuja Gairo hapa, nitakuja na Afisa madini wa Mkoa, chagueni wawakilishi kumi baina ya wanunuzi na wachimbaji wadogo na hii Leseni isimame kwanza hadi tutakapoafikiana juu ya utaratibu wa hapa” amesisitiza Shigela.
Pamoja na kusitisha leseni hiyo na kuwataka watu wachimbaji kuendelea na utaratibu wa awali wa kuchimba madini Shigela amewataka wachimbaji hao kufanya biashara hiyo kwa kufuata miongozo yote ya kiserikali ili Serikali nayo iweze kupata mapato yake.
RC Shigela akitoa leseni ya umiliki wa sehemu ya eneo la uchimbaji madini muda mfupi kabla hajasimamisha matumizi ya leseni hiyo
Onyo la RC Shigela kwa wachimbaji na wafanya biashara wa madini
“Ni kinyume cha Sheria na ni kosa kubwa sana kuiba madini, kutorosha madini na kwenda kuuza katika utaratibu usiokubalika katika nchi yetu”. Ameonya Shigela.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabiri Omary Makame pamoja na kuwapongeza wachimbaji madini kwa kushiriki kutoa tozo na ushuru wa aina mablimbali kupitia madini hayo, amemuomba Mkuu wa Mkoa kuingilia kati suala la changamoto za miundombinu ya barabara na ukosefu wa maji safi na salama suala ambalo Mkuu wa Mkoa amemuagiza Meneja wa TARURA na Meneja wa RUWASA Wilayani humo kushughulikia kero hizo mara moja.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabil Makame (katikati) akishuhudia RC akitoa leseni ya umiliki wa eneo la uchimbaji wa madini
Kamishina Msaidizi mwandamizi wa Polisi Fortunatus Musilimu ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro amewahakikishia wachimbaji wa madini wa Kitaita ulinzi imara katika eneo la mgodi huku akiwaomba kutoa ushirikiano wao kwa jeshi la Polisi kwa kuwa watu katika eneo hilo ni wengi hivyo unatakiwa ushirikiano wa dhati na kulazimika Kamanda huyo kutoa namba yake simu ya kiganjani kwa ajili ya mawasiliano zaidi.
Afisa Madini Wilaya ya Gairo Tito Mahela amefafanua suala la bei ya uuzaji wa madini kuwa bei elekezi ya kununua madini katika eneo la uchimbaji ni shilingi 100,000/= hata hivyo yule asiyeridhika na bei hiyo afuate utaratibu wa kupata kibali ofisini kwake ili kwenda kuuza madini yake katika soko ambalo lipo Kisheria Wilayani Gairo ambapo dhahabu itanunuliwa kwa shilingi 123,000/=
Afisa Madini Wilaya ya Gairo Titus Mahela (katikati)
Aidha wachimbaji wa madini baada ya kusikilizwa kero zao ambazo zilipewa majibu sahihi, wameiomba Serikali isiwasahau kwenye zoezi la sense ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu, kwa kuwa wamesema muda huo wao watakuwepo eneo la machimbo kwa kuwa hizo ndio shughulia zao za kila siku lakini wanaomba kuhesabiwa.
Umati wa wachimbaji wa madini eneo la Kitaita waliokusanyika kutoa kero zao kwa Mkuu wa MKoa
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.