Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Pascal Kihanga kutenga eneo lenye hekari 4,500 kwaajili ya kuwagawia viwanja vijana wa timu ya Mtibwa Suger wenye umri chini ya miaka 20 walioshiriki michuano ya ligi ya vijana mwaka huu.
Shigela ametoa agizo hilo Juni 22, mwaka huu wakati wa hafla ya kuwapokea mabingwa hao wakitokea Dar es Salaam hafla iliyofanyika Bwalo la Umwema katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro baada ya vijana hao kuibuka mabingwa wa mashindano hayo mara tatu mfurulizo katika michuano ya ligi ya vijana chini ya umri huo.
Mkuu wa Mkoa Martine Shigela ametoa ametoa agizo la vijana hao kupewa viwanja ili kuwaenzi wachezaji hao, na kwa kufanya hivyo watakuwa wametoa hamasa kwao na kuthamini mchango wao katika tasnia ya michezo.
‘’..watengeneze mtaa kuenzi timu hii katika Mkoa wetu na Manispaa yetu tunauita MTAA WA MTIBWA SUGER AU MTIBWA SPORTS halafu wanajenga nyumba zao pale, sasa mstahiki meya nadhani umenielewa na DC, mkubwa huwa haombi anaongea kidiplomasia lakini ameagiza hivyo…’’ amesema Shigela.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Halima Okash amewatia moyo mabingwa hao akiwaeleza umuhimu wa michezo ambapo amesema mpira ni Afya, mpira ni ajira lakini pia mpira unawasaidia kutambulika kitaifa na kimataifa kwa kujuana na watu mbalimbali katika sekta ya michezo.
Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Wilaya amesema ameahidi kuwa bega kwa bega na timu hiyo katika kuiunga mkono na kuitangaza ili iweze kufika pale ambapo inatarajia.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoani humo (MRFA) Pascal Kihanga ametoa wito kwa viongozi wa timu ya Mtibwa suger kutowazuia wachezaji hao vijana kusajiliwa na timu nyingine pale wanapohitaji kusajiliwa kwa kuwa hiyo ndiyo ajira yao.
Hata hivyo Pascal Kihanga ametahadharisha kuwa jambo hilo pamoja na kuwa litaleta sifa ndani ya Mkoa wa Morogoro na timu ya Mtibwa suger kwa kuonekana kuwa ni kiwanda cha kuzalisha wachezaji lakini litafutiwe utaratibu unaofaa katika maana ya kuwa na mikataba yenye kuleta faida kwa pande zote tatu yaani club inayouza, inayonunua na kwa mchazaji mwenyewe.
Mkurugenzi wa Mtibwa Ndg. Abel Magesa amesema wachezaji hao huchukuliwa wakiwa wadogo kutoka maeneo mbalimbali ambapo wanalelewa na kutunzwa kwa gharama kubwa wakiwa na imani ya kupata wachezaji wazuri hapo baadae ambao mara nyingi husajiliwa na kuchezea timu kubwa za hapa nchini zikiwemo timu ya Yanga na Simba.
‘’Tumekuwa kisima cha kutoa wachezaji mashuguri kwenye vilabu vya Simba na Yanga na hata timu nyingine mashuhuri, kwa sababu wanajua Mtibwa Suger ni kina cha kuchota maji kwa ajili ya kandanda’’ amesema Magesa.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, msemaji wa timu ya Mtibwa Suger Thobias Kifaru ameeleza kuwa timu yao ni chuo cha kuandaa wachezaji wa mpira wa miguu, huku wachezaji wa kikosi hicho akiwemo Abdul Kapirima na Frank George wametoa pongezi zao kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa mapokezi mazuri ambayo hayakuwahi kutokea na kuahidi kuongeza juhudi ili kuendelea kuchukua ubingwa kwa mashindano yajayo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.