Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewapongeza Viongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa Mshikamano mzuri katika utekelezaji wa Miradi ya Kimaendeleo kwenye Halmashauri ya Manispaa hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akikagua Jengo la Wagonjwa wa Dharura lililopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo wakati wa Ziara yake ya Kikazi iliyofanyika Mei 18 Mwaka huu.
Martine Shigela ameyasema hayo Mei 18 Mwaka huu wakati wa Ziara yake ya Kikazi ya Kukagua Miradi ya Maendeleo katika Halmashauri hiyo ikiwemo kukagua matumizi bora ya fedha za Mapato ya ndani na zile za Serikali Kuu za Miradi Mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri hiyo.
Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa amefarijika kuona utekelezaji wa maagizo ya kamati ya Bunge ya kila Halmashauri yenye mapato makubwa kujenga kituo kimoja cha Afya na madarasa kadhaa ili kuinua Shule za msingi unaendelea vizuri ikiwemo ukamilishaji wa miradi hiyo katika kata za Tungi na Lukobe katika Manispaa hiyo.
“Kwa hiyo mimi nimefurahi kuona kwamba Maagizo ya Kamati sasa tunajenga kituo cha Afya tayari milioni 250 zimekwishaletwa hapa kupitia mapato yenu ya ndani, nawapongeza kwa hilo” amesema Shigela.
“Lakini nimefarijika zaidi kuona kwamba katika Mapato yenu ya ndani nje ya kujenga Kituo kimoja cha Afya mmekamilisha ujenzi wa Zahanati sita na Madarasa 53 ambapo kati ya hayo yalitokana na mapato ya ndani ni 45, hayo ndio mambo ninayotaka kuyaona katika Manispaa hii” ameongeza Shigela.
Katika hatu nyingine Martine Shigela amemuelekeza Mkurugenzi Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Msimamizi wa mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Lukobe kinachojengwa kutokana na fedha za tozo Tsh. 1.2Bil. kumsimamia vema Mkandarasi wa Ujenzi huo ili kukamilisha ujenzi huo kabla au ifikapo June 30 Mwaka huu.
Kwa upande wake Meya wa Halmashauri hiyo Mhe. Paschal Kihanga amebainisha kuwa Miradi ya Elimu na Afya iliyokamilika na inayoenda kukamilika inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi kulingana na kada husika hivyo, amemuomba Mkuu wa Mkoa kushughulikia changamoto hiyo ili wananchi waweze kuhudumiwa kikamilifu.
Naye Diwani wa Kata ya Lukobe Mhe. Celestine Mbilinyi ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za ujenzi wa Kituo hicho ili kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi wa eneo hilo.
Hadi sasa kiasi cha Shilingi milioni 250 zimekwishapelekwa kituoni hapo kwa ajili ya kuharakisha ujenzi huo wa kituo nhicho ambacho umefikia asilimia 75% ya kazi hiyio.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.