RC Shigela awatoa hofu Wanamorogoro kuhusu chanjo ya UVIKO – 19.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewatoa hofu wakazi wa Mkoa huo na watanzania wote kwa ujumla kuhusu chanjo ya UVIKO – 19 huku akieleza kuwa chanjo hiyo ni salama na inalenga kuokoa maisha ya watanzania na si vinginevyo.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wakiwa kwenye kikao
Shigela ametoa rai hiyo wakati akifungua kikao cha uhamasishaji wa chanjo ya UVIKO – 19 kwa wawakilishi wa Taasisi mbalimbali zilizopo Mkoani humo zikiwemo taasisi za kidini kwa lengo la kupata elimu ya chanjo hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Wajumbe kutoka taasisi mbalimbali walioshiriki kikao hicho
Amesema, propaganda zinazotolewa na baadhi ya mitandao ya kijamii kutoka kwa baadhi ya watanzania sio za kweli na zinalenga kudhoofisha Afya za Watanzania na juhudi za Serikali za kupambana na ugonjwa wa UVIKO – 19.
“yamekuwepo maneno hasa kwenye sekta hii ya chanjo dhidi ya CORONA kulingana na tafasiri mbalimbali za watu… wakiwa na nia ileile ya kutaka kudhoofisha Afya za Watanzania lakini pia kurudisha nyuma jitihada za Serikali ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan za kupambana na ugonjwa wa CORONA” alisema Martine Shigela.
wakati wa Kikao wajumbe walipewa Elimu ya chanjo ya UVIKO - 19
Katika hatua nyingine, Shigela amewataka viongozi wenzake kusimamia suala hilo kwa umakini huku akiwatoa hofu kuwa chanjo hiyo ni salama na ina nia njema na watanzania na kubainisha kuwa yeye ndiye mtu wa kwanza kupata chanjo ya UVIKO – 19 katika Mkoa wa Morogoro hivyo watu wasiwe na hofu bali kila mmoja kwa hiari yake achukue jukumu la kwenda kuchanja.
Taasisi za Serikali na Vyamba vya siasa pia walishiriki kikao hicho
Mratibu wa UKIMWI Mkoa wa Morogoro ambaye pia ndiye mratibu wa Chanjo ya UVIKO – 19 Mkoa wa Morogoro Dkt. Masumbuko Igembya ameeleza lengo la kikao hicho kuwa ni kuendelea kuweka mikakati madhubuti ya zoezi hilo la chanjo ili watu waepukane na ugonjwa wa UVIKO – 19.
Aidha, Dkt. Masumbuko amesema faida Msingi na kubwa ya chanjo ya UVIKO - 19 ni kupunguza madhara makubwa ya ugonjwa huo iwapo mtu ataambukizwa chanjo itamsaidia aindelea kuwa salama.
Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Morogoro Dkt. Masumbuko Igembya akisikiliza kwa makini maswali ya wajumbe ili ayatolee ufafanuzi
Kwa upande wao washiriki wa kikao hicho akiwemo Askofu Jacob Mameo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania - KKKT Dayosisi ya Mashariki amewataka watanzania wasidanganyike na maneno ya kwenye mitandao kwamba chanjo hiyo sio salama, kwani amesema hakuna kiongozi wa Serikali Duniani anayeweza kudiliki kudhuru watu wake huku akishuhudia kuwa yeye pia amechanjwa chanjo hiyo na afya yake iko vizuri.
Viongozi kutoka Taasisi za kidini wakisikiliza kwa makini Elimu ya Chanjo ya Uviko - 19
Katibu wa Baraza la Wazee Mkoa wa Morogoro Bakili Anga, yeye amekwenda mbali zaidi kuwa pamoja na chanjo hiyo ina malengo ya kupambana na ugonjwa wa CORONA bado ina faida zaidi kwani kabla ya kuchanja chanjo ya COVID – 19 alikuwa anasumbuliwa na homa ya malaria kila baada ya miezi sita lakini mara baada ya kuchanjwa hajapata homa hiyo ya malaria.
Naye katibu wa BAKWATA Mkoa wa Morogorom Ahmad Khairalah ameeleza kuwa kutokana na elimu aliyoipata katika kikao hicho amewataka watanzania wajitokeze kwa wingi kupata chanjo ili wajikinge na afya zao ikiwa ni kwa manufaa yao na wengine.
Kwa mujibu wa Dkt. Masumbuko Igembya, Halmashauri ya manispaa ya Morogoro inaongoza kwa wananchi wake kuhamasika kwa kupata chanjo kwani hadi sasa watu 5,051 wamechanjwa sawa na asilimia 72 ya wananchi wanaotakiwa kuchanjwa katika Halmashauri hiyo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.