RC SHIGELA AWATWISHA ZIGO WAKUU WA WILAYA.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mkoa huo kupiga marufuku Walimu wa Shule kuwasimamisha masomo wanafunzi kwa kigezo cha kutolipa michango mbalimbali ya Shule kwa kuwa Serikali imekwishalipa Michango hiyo.
Kabla ya kufanya mkutano na wananchi Mkuu wa Mkoa alitembelea mitaa michache ya Kata ya Dakawa kwa ajili ya kukagua zoezi la Anwani za Makazi na uwekaji wa vibao vya kuonesha barabara na mitaa ambalo kwa Wilaya ya Mvomero liko katika hatua za mwisho. Hapa Mkuu wa Mkoa akibandika kibao kinachoonesha anwani ya makazi kwenye jengo la makazi mmoja.
Martine Shigela ametoa agizo hilo Mei 17 Mwaka huu wakati akiongea kwenye mkutano wa hadhara na Wananchi wa Kata ya Dakawa wakati wa ziara yake ya siku moja Wilayani Mvomero ambapo pamoja na mambo mengine Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa hakuna sababu za msingi za watoto kukatazwa kuingia darasani kwa ajili ya kusoma kwa sababu ya kukosa michango hiyo.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kwamba ni aibu kwa Mwalimu kumsimamisha masomo mwanafunzi kwa sababu ya michango walio kubaliana wazazi kuchanga wakati Serikali inato fedha kwa ajili ya Elimu bila malipo kila Mwezi ili watoto wapate kusoma bila kubugudhiwa na yeyote.
“niombe na kuelekeza kwa Wakuu wa Wilaya ni marufuku, ni marufuku, ni marufuku, ni marufuku kwa Mwalimu kumzuia mtoto Shule kwa Michango ya kuchangishana mliokubaliana na Wazazi…” amesema Shigela.
“Kila mchango mtakaokubaliana lazima ukapate kibali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya na kibali hicho kikitoka lazima kikasimamiwe na Mkurugenzi wa Halmashauri” amesema Shigela.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza wataalamu wa Elimu katika Shule zote Shikizi ambazo zimepelekewa fedha za maendeleo kwa ajili ya Shule hizo zikamilishe usajili wake mapema ili kuwa Shule kamili kwa lengo la kuondoa usumbufu kwa wanafunzi na wananchi kutokana na changamoto ya kuwa mbali na maeneo wanayotoka wananfunzi hao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Bi. Halima Okashi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zaidi ya Shilingi milioni 563 kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya kiwango cha Lami ndani ya Kata hiyo ili kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.
Mkuu huyo wa Wilaya amebainisha kuwa hadi sasa Serikali katika kata hiyo imetoa kiasi cha Shilingi milioni 207 kwa ajili ya kutatua kero ya miundombinu ya Maji katika Kata hiyo ya Dakawa ambapo hadi sasa kwenye sekta ya maji maeneo mengi ya miradi ya maji wako katika hatua ya ulazaji wa mabomba na fedha zingine zaidi ya bilioni 2 ili kusaidia utatuzi wa kero hiyo katika Kata ya Dakawa.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Bi. Halima Okashi
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambaye pia ni Diwani wa Kata hiyo Mhe. Yusuph Makunga ameishuruku Serikali ya awamu ya Sita kwa kutatua kero mbalimbali katika Kata hiyo ikiwemo kutoa kiasi cha Shilingi milioni 100 kwa ajili ya shule Shikizi ya Maji Chumvi, Shilingi milioni 60 katika Shule Shikizi Mtakuja katika Kijiji cha Wami Luhindo na Shilingi milioni 60 katika Shule ya Sekondari ya Dakawa.
Diwani wa Kata ya Dakawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mhe. Yusuph Makunga akieleza kero za wananchi wa kata yake
Kwa upande wao wananchi wa Dakawa akiwemo Mariam Pantaleo amesema tatizo kubwa linalowakabili Mvomero ni uwepo wa mashamba pori mengi ambayo wamiliki wake hawayafanyii kazi wakati huo huo wananchi wanakosa maeneo ya kufanyia shughuli za kijamii ikiwemo makazi, kilimo na ufugaji.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Dakawa
Aidha, Bi Mariam amesema licha ya uwepo wa mashamba pori hayo lakini pia kuna udanganyifu unaofanywa na wenye mashamba hayo ambapo ukubwa wa ekeri unaooneshwa kwenye hati miliki ni tofauti na uhalisia wa ukubwa uliopo na kama mashamba hayo yatapimwa itakuwa karibu mara mbili ya ukubwa unaoonekana kwenye hati zao jambo ambalo Mkuu wa Mkoa ameahidi kutuma wataalamu wake kufanya uchunguzi wa suala hilo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.