RC Morogoro kuunda timu kuchunguza upotevu wa dawa, awanyooshea kidole watumishi wasio waaminifu
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela yuko mbioni kuunda timu ya kuchunguza upotevu wa dawa zinazoletwa na Serikali Mkoani humo na kuwaonya watumishi wa Serikali wasiowaaminifu katika utendaji wao kubadilika, vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria na kinidhamu.
Martine Shigela ametoa kauli hiyo Julai 23 mwaka huu alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili Wilayani Kilosa katika vijiji vya Msowero, Mvumi na Mji wa Kilosa kwa lengo la kujitambulisha, kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.
Akizungumzia suala nzima la upotevu wa dawa Mkuu huyo wa Mkoa amesema haiingii akilini fedha zinaletwa na serikali katika vituo vya kutolea dawa lakini wananchi hawapati dawa, na kwamba jambo hilo hatalivumilia kwa kipindi chake chote cha Ukuu wa Mkoa ndani ya Mkoa huo.
“haiingii akilini fedha zinaletwa, wananchi hawapati dawa,jambo hili sitalivumilia katika uongozi wa kipindi changu nikiwa Morogoro” alionya Martine Shigela.
“kama dawa zinaletwa, Mhe. Rais Samia anawaletea fedha, mnanunua dawa, na mkinunua dawa baada ya siku mbili…dawa zimeisha, mjiandae kuzitapika hizo fedha za dawa ili dawa zinunuliwe tuweze kujiendesha katika zahanati zetu” aliongeza Mhe. Shigela.
Amesema, haiingii akilini, Serikali inajenga Hospitali za Rufaa, Hospitali za Wilaya, vituo vya afya na zahanati kwa kutumia fedha za ndani na kuongeza bajeti ya dawa kutoka Bil. 38 mwaka 2015 hadi Bil. 300 mwaka jana halafu dawa ziendelee kutopatikana, hivyo amewataka wahusika wote wa idara ya Afya Mkoani humo kujipanga na kutafuta njia ya kuondoa changamoto hiyo.
Kwa sababu hiyo amesema ataunda timu ambayo itapita kwenye Hospiatli za Wilaya zote, Vituo vyote vya Afya vyote na Zahanati zote za Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kuchunguza mtandao unaohusika na kupoteza dawa hizo zinazoletwa na Serikali.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri, Mkuu huyo wa Mkoa amesema ni wajibu wa kila Halmashauri kukusanya mapato yake kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vilivyoko katika halmashauri husika, hata hivyo amesema wapo watumishi wachache wasio waaminifu ambao baada kukusanya fedha hizo wanazitumia.
Ili kudhibiti hilo, Mkuu wa Mkoa Martine Shigela ametoa utaratibu mpya utakaotumika kwa mkoa mzima, kwa watendaji wa Kata kupeleka kwa Wakuu wao wa Wilaya, taarifa ya makusanyo ya fedha zinazokusanywa ndani ya kata zao kutoka kwenye vyanzo mbalimbali kwa kutumia mashine (POS) ili wale wanaohusika kutowasilisha fedha za makusanyo washughulikiwe mapema badala ya kutengeneza madeni makubwa.
“nataka kila wiki mpeleke kwa Mkuu wa Wilaya kwenye kila kata, watu wako wanaokusanya fedha kwenye system, wanasomeka wamekusanya milioni mbili na mpaka leo wamepeleka zote benki, watu wako kwenye kata wako wanane wana pouse wamekusanya milioni nane lakini kwenye nyaraka wanaonesha wamepeleka milioni sita ili milioni mbili wazitapike mara moja ndani ya hiyo wiki” ameelekeza Shigela.
Amesema, wananchi wanachelewa kupata maendeleo yao kwa sababu tu ya viongozi wachache kushindwa kusimamia vizuri makusanyo ya fedha hizo. Martine Shigela ametumia fursa hiyo kuwaagiza Wakurugenzi watendaji wote Halmashauri za Mkoa huo kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato yao ya ndani.
Kuhusu kero za migogoro ya Ardhi Wilayani Kilosa Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi kutulia wakati timu kutoka Wizarani inayoinisha mipaka ya mashamba yaliyorudishwa Serikali inaendelea kwa ajili ya kuwagawia wananchi huku akitaka Jamii ya wafugaji wanaojichukulia sheria mikononi kwa kuwapiga na kuwaua wakulima kuacha kufanya hivyo kwa kuwa wakithibitika sheria haitawaacha salama.
Afisa Ardhi Wilaya ya Kilosa Nkelege Cheyo amewaomba wananchi wa Wilaya hiyo kutoa ushirikiano wa dhati katika zoezi la uainishaji wa mashamba ili likamilike haraka kwa kuwa zoezi hilo kwa sasa linafanywa chini ya usimamizi wa polisi jambo ambalo amesema halina afya wala halikubalika.
Nao wananchi wa kijiji cha Majambaa kupitia Nuhu Maulid Ngae walimwomba Mkuu wa Mkoa huo kumuachia Mwenyekiti wa Kijiji chao na wajumbe wake sita ambao walikamatwa na kuwekwa rumande kwa sababu zisizojulikana jambo ambalo Mkuu wa Mkoa alilikubali na kuagiza jeshi la polisi kuwaachia viongozi hao huku akiwataka waache kupingana na Serikali bila kufuata utaratibu.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Lucas Asajile Mwambambale alimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa Mwenyekiti Njile Jibusa pamoja na viongozi wengine sita walikamatwa kwa sababu ya kuingilia kazi inayofanywa na timu kutoka Wizara ya Ardhi ya kuainisha mipaka na matumizi ya shamba la Mbugani Estaste kwa kung’oa baadhi ya almama (bicon) zilizowekwa na timu hiyo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.